https://foundation.mozilla.org/en/what-we-fund/awards/common-voice-kiswahili-awards/

Mashindano ya uandishi: Washindi wa awamu ya Kwanza

Baada ya takriban wiki sita za kupokea miswada iliyowasilishwa kwa mashindano na pia mchakato wa kutafuta na kuamua mshindi, ni furaha kubwa kuwaletea washindi wa awamu ya kwanza ya haya mashindano,

Miswada iliyowasilishwa ilikuwa ya kiwango cha juu sana na uamuzi wa kuteua washindi hawa watatu haikuwa kazi rahisi maanke kazi nyingi zilistahiki kushinda. Hili ni jambo ambalo latia moyo sana, kuona kwamba waandishi wa Kiswahili wanajikakamua na kuandika kazi za kiwango cha juu, japokuwa warsha za uandishi na uchapishaji wa riwaya kwa Kiswahili ni chache mno.

 

Mshindi wa tatu: Elias B Shelukindo (Tanzania)

Elias B Shelukindo aliyezaliwa mwaka terehe 2 Juni mwka wa elfu mbili na mbili ni mwandishi kutoka Manyara Tanzania. Pia ni mwanafunzi katika chuo cha Elimu ya Biashara Dodoma, ngazi ya stashahada. Kwa kujieleza, anasema kuwa ni ‘mwandishi chipukizi katika uwanja wa fasihi.’

Insha yake kwa anwani Barua Kutoka Mtaani ni kazi ambayo inaangazia masaibu ya Watoto wa mitaani. Kutoka pale mwanzo, “Fungueni pazi mtazame filamu ya ghazabu…” mwandishi anaeleza masaibu ya Watoto wa mitaani, namna ambavyo watoto wa kike hubakwa wakiwa wangali Watoto, kufikia hali ya “mtoto kuzaa mtoto” na hali ya kutatanisha ya watoto hawa wa mitaani kuuzwa kama bidhaa katika biashara ya binadamu. Insha yatiririka vizuri na mwandishi anatumia sentensi fupi fupi kuendesha kisa, sentensi ambazo muundo wake umefaa kabisa kwa kazi hii.

Kazi hii ilifika kwa tatu bora kwa kuwa inazungumzia swala la utu na kwa upana uanaharakati katika jamii ikizangatiwa kuwa sote ni wamoja ata kama hali zetu za kimaisha ni tofauti. Tutakuacha na kauli hii kutoka Barua Kutoka Mtaani;

“…Basi kama tumekubali kushindwa kuwalinda dhidi ya mbu wakali wanaowapatia malaria, basi tuwalinde dhidi yah ii hatari ya biashara ya binadamu.”

 

Mshindi wa pili: Omar Kibulanga (Kenya)

Omar Kibulanga ni mbunifu anayependa kufanya kazi za Kiswahili kwa ajili ya mapenzi yake kwa lugha hiyo pamoja na utajiri wa turathi za Uswahili. Ana hadithi, mashairi, filamu na makala mbalimbali ambayo yanapatikana hususan kupitia akaunti zake kwenye mitandao kama vile Facebook, Instagram na YouTube – Omar Kibulanga. Aidha mashirika mbalimbali yamefaidi huduma zake, mathalani MNET, Supersport, BBC, Royal Media Services, Nation Media Group pamoja na taasisi kadha za kiserikali nchini Kenya.

TETE SERIES EPISODE 1 – HABIB SWALEH ndio kazi yake ya hivi karibuni. Hii ni filamu ya wasifu wa Habib Swaleh, msomi na mwana-mageuzi wa kipekee aliyevuma kisiwani Lamu nchini Kenya kwa kuchangia pakubwa katika sekta za elimu, sayansi na utamaduni na kuacha athari nzuri zilizoenea katika mwambao wa Afrika Mashariki na kwingineko.

Riwaya yake Mapend’i T’ungu-nzima imepata nafasi hii ya pili. Kupitia kichwa cha riwaya hii fupi, ni wazi kwamba mwandishi amechagua lahaja ya Kiamu, jambo ambalo lilifurahisha majaji, kuwa kuna waandishi ambao wamezingatia umuhimu wa kuhifadhi lahaja za Kiswahili na sio tu kuandika kupitia lugha iliyosanifishwa. Hivi, kazi ya Kibulanga imeonekana kuwa muhimu sana katika muktadha wa uandishi wa Kiswahili kudumisha na kuhifadhi lahaja zake.

Mapend’i T’ungu-nzima ni riwaya ambayo imechukua muundo wa hadithi asili kutoka pwani ya Kenya kwa kuwasilisha maana tofauti kwa msomaji. Riwaya inaanza kwa mandhari ya kifo cha mfalume wa milki ya Lamu, na waziri mwaminifu aliyekuwa tayari kuukoboa moyo wake kifuani ili ubandikizwe kwenye kifua cha yule mfalume mahututi, kisha yeye awekwe pera pahala pa moyo wake.

Safari ya waziri kuchunguza kwa kina vita na kifo cha yule mfalume ikampelekea kwa watu tofauti, kila mmoja akimwelekeza kwa mwingine ambaye alidhaniwa kuwa atajua zaidi kuhusu hali hii. Riwaya inamalizika kwa nyumba ya bwana mmoja na mkewe na hali ya kumkaribisha waziri.

Uamuzi wa mwandishi kutumia lahaja kuandika hii riwaya imetia ladha aina yake, na riwaya yenyewe imesukwa kwa muundo ambao ni nadra sana kukutana nao katika fasihi. Kwa mfano, tazama sentensi hii:

“N’ke wangu namna gani? Amekuya n’geni hata tanga(butternut) hukun’katia…” Mume alitanguliza kabla ya kumkongowea mgeni wake.

La pili, kwa mtazamo wetu (na hapa kila mwandishi huenda akawa na mtazamo tofauti kulingana na namna mwandishi ametunga kazi hii) ni kuwa mwandishi ameangazia umuhimu wa mwanamke katika jamii. Hekima huota kwa moyo latifu, na hapa, mwanamke amejitokeza kuwa mwenye hekima na busara kupitia upole wake. Hii ni ishahara au ushahidi kuwa chuo cha kwanza ni chini ya mama mlezi, na hapa ndio chanzo cha utu, hekima na busara.

Tungependa kusoma kazi zingine zilizoandikwa kwa lahaja tofauti za Kiswahili. Huu uanharakati wa fasihi utachangia pakubwa kuhifadhi hizi lahaja.

Kabla kutaja washindi, itakuwa vyema kumpa hongera mwandishi Leonidas Bigirimana ambaye aliwasilisha kazi aliyotafsiri kutoka Kirundi kuleta kwa Kiswahili. Kazi yenyewe kichwa chake ni Uchunguzi wa Ngoma za Kitamaduni na Usawiri wa Jinsia Nchini Burundi na kwa kweli sio rahisi kutafsiri kazi ya kurasa sabini na tano kutoka lugha moja kwenda nyingine.

 

Mshindi wa kwanza: Florence Chanya Mwaita

Florence Chanya Mwaita ni mtaalamu wa mawasiliano, mwandishi, mhariri, malenga, na mpenzi wa lugha ya Kiswahili. Ana shahada ya mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Daystar. Alikuwa mhariri mkuu wa Gazeti la Involvement lenye Jamvi la Kiswahili. Hali kadhalika alitafsiria na kuandikia Etaarifa, pamoja na kutoa mchango wake kwenye ukumbi wa mashairi wa Taifa Leo; miongoni mwa majarida mengine. Ikiwa haandiki, anasoma, la sivyo, anafuma.

Riwaya ya Florence, Mdudu Mbaya Zaidi ambayo imeshinda nafasi ya kwanza imewasilishwa kwa wakati unaofaa kabisa. Riwaya inaangazia wanasiasa kwa kutumia sitiari ya nyigu kupe (kama mwanasiasa mbinafsi), mdudu ambaye hutaga yai lake ndani ya buibui aina ya tarantula,.

“…Aisee sitii chumvi, nyigu kupe humwandama buibui bila huruma, humvamia akamchoma kwa mwiba wake wenye sumu inayolemaza. Akilegea tu nyigu humpara mgongoni akataga yai lake ndanimwe kisha humburura hadi mafichoni, anapomuacha baada ya kuziba tundu alilopekecha. Ikumbukwe kuwa buibui wa aina ya tarantula ni mkubwa zaidi ya nyigu na ni mzito sana ikilinganishwa na kidudu kinachomtendea unyama huo. Hali kadhalika, buibui mwenyewe ni hatari; lakini ataachwa hoi, hajui kilichomkuta, hana tofauti na aliyekufa, na kifo chake ni taratibu na kichungu zaidi…”

Sasa hivi shughuli na kampeni za kisiasi zimefika kileleni hapa Kenya na uchaguzi mkuu umekaribia. Wanasiasa wanazunguka kila mahali kwa magari yao ya kifahari au kwa njia ya helikopta, na wananchi maskini wanapewa pesa kidogo-kidogo ili wahudhurie hizi kampeni. Gharama ya Maisha imepanda maradufu lakini mwanasiasa ni yule yule na ahadi zake zisizotimizwa.

Kwa kweli, kama mwalimu Abdilatif alivyosema katika shairi lake, mwenye lake hawati!

Florence anaeleza kuwa ata kama nyigu kupe ni mdudu mbaya, faida zake zipo, lakini mwanasiasa mbinafsi ni mbaya zaidi maaanke hana faida yoyote. Anahitimisha riwaya hii nzuri kwa maneno haya:

“…Lakini kwa sasa mimi ni mwandishi, na nadhani nimeutumia wino wangu huu vizuri. Ndiko kukaa ange huku, la sivyo, mdudu mbaya zaidi atahakikisha sina ruhusa ya kuitumia lugha ya Kiswahili katika uandishi! Na hapo sitalemaa tu, atakuwa ameitoa roho yangu.”

Shukrani zetu kwa Mozilla Foundation kwa kuwezeshe mashindano haya. Sana tungependa kusisitiza umuhimu wa kuwa na mashindano kama haya yanayohusisha uandishi kwa lugha ya ya Kiswahili na lahaja zake, na pia warsha ambazo zitasaidia kupoiga msasa kazi kwa hizi lugha na kukuza kizazi cha wapenzi, wasomaji na waandishi wa Kiswahili.

Feature Photo Credit

 

 

 

Abdilatif Abdalla, Common Voice, kiswahili, Mozilla Foundation


Hekaya Initiative

Writing the East African Coast.

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

© Hekaya Initiative 2018-2020. All Rights Reserved. Design by Crablinks
%d bloggers like this: