Bibi Titi Mohamed, Mama Wa Taifa

Na Rahma Mkai

Mama wa taifa kwa umaarufu anajulikana kama Bibi Titi Mohamed. Alizaliwa mwaka elfu moja mia tisa ishirini na sita katikati mwa jiji la Dar es Salaam kwenye familia ya Kiislamu. Kama wenzake wengi wa wakati huo, hakupata elimu rasmi, lakini alijifunza mengi kutoka kwa wazazi wake na familia yake kwa jumla. Katika miaka ya elfu moja mia tisa na hamsini, alikuwa ni miongoni mwa wale waliopigania uhuru wa Tanganyika kutoka ukoloni wa Uingereza akiwa pamoja na Mwalimu  Julius Nyerere, chini ya mwamvuli wa chama cha Tanganyika African National Union. Bibi Titi alikuwa na maneno makali dhidi ya ukoloni na alikuwa ana nguvu kubwa ya kushawishi. Akiwa na miaka kumi na sita tu alikuwa mmoja kati ya wanawake wachache walioaminiwa katika kuongoza mapambano dhidi ya udhalimu waliokuwa wakifanyiwa watanganyika.

Watanzania Kumbukumbu pekee tulinayo ya Mwanaharakati huyu katika taifa letu ni mtaa na Barabara ya Bibi Titi iliyopo Dar es salaam. Kihistoria Bibi Titi Mohammed aliingia katika siasa kwa kushawishiwa na Schneider Plantan, akapewa kadi namba kumi na sita, na mumewe bwana Boi Selemani alipewa kadi namba kumi na tano. Alikuwa ni muasisi wa Umoja wa wanawake Tanganyika uliokuja kuundwa rasmi Mwaka elfu moja mia tisa sitini na tatu. Wakati wa harakati za kupigania Uhuru alisimamia vikundi vya muziki kama vile ‘Lele Mama’ na mara zote alitangulia kuongea na umati mkubwa wa watu Kabla hata ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere hajaongea. Aiaminika sana na watu.

Umaarufu wa Bibi Titi aliupata kupitia ukombozi wa wanawake. Alikuwa ni mwanamke wa kwanza kujiunga na harakati mbalimbali za kupigania uhuru wa Tanganyika. Mwanzoni mwa harakati zake za kisiasa, alifanikiwa kulishawishi kundi kubwa la wanawake kujiunga pamoja naye. Kama kiongozi wa tawi la wanawake la chama cha Tanganyika African National Union, alikuwa na jukumu la kuwashawishi wanawake wenzake kuunga mkono maoni na sera za Tanganyika Africa National Union. Bibi Titi Mohammed katika harakati zake za kuwakomboa wanawake alikaririwa siku moja akisema; “dhumuni langu kubwa ni kuhakikisha naamsha akili za wanawake waliolala na kubadilisha fikra na mitazamo yao na kuwaaminisha kwamba Uhuru wa Tanganyika utapatikana kama wanawake watajitambua.” Alikua na lugha ya ushawishi sana.

Mnamo mwaka elfu moja mia tisa na hamsini na tano, Mwalimu Nyerere na Bibi Titi walifanya mkutano mkubwa huko Tabora. Hii ni kutokana na mualiko walioupata toka kwa watu wa huko. Ikumbukwe kuwa Tabora ya wakati huo ilikuwa na hamasa kubwa Katika kudai Uhuru. Hivyo mualiko ulitoka kwenye kamati ya wazee kama Hassan Mohamed Ikunji, Hamisi Khalfani, Swedi Mambosasa, Germano Pacha, Juma Mrisho, Shaaban Mohamed Silabu, Bilali Rehani, Waikela, na Mohamed Mataka, wakati ule akiwa mwadhini wa Masjid Nur— msikiti wa Wamanyema pale mkoani Tabora.

Katika mikutano mingi ya harakati za Uhuru aliyoongoza Bibi Titi Mohammed mfano ni ule wa Mombasa alioshirikiana na Tom Mboya wa Kenya, katika ukumbi wa Tononoka. Kiujumla Mkutano Mkuu wa kwanza Tabora ulifungua njia kukubalika kwa Tanganyika African National Union. Baadaye kulifanyika Azimio la Tabora. Azimio hilo liliongozwa na Mwalimu Nyerere na wengine kama Sheikh Suleiman Takadir, Mzee Jumbe Tambaza, Juma Selemani na Bibi Titi. Hivyo Bibi Titi alikuwa mmoja wa waasisi wa Azimio la Tabora na mwanamke pekee kuwa katika nyadhifa hiyo. Baada ya uhuru wa Tanganyika na katika miaka ya mwanzo ya kuundwa kwa Tanzania, muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Bibi Titi alipewa uwaziri chini ya uongozi wa Wilaya mbili— Wilaya ya Rufiji na Wilaya ya Mufindi, na baadae alichaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa wanawake Tanganyika na baadae waziri. Halikuwa jambo la kushtua kwani alistahili na pia alikua na uwezo.

Katika mwaka elfu moja mia tisa sitini na tatu, inaelezwa kulitokea kutoelewana kati ya Bibi Titi na Mwalimu Nyerere wakati wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Tanganyika Africa National Union uliofanyika ukumbi wa Karimjee, Dar es salaam. Hapo walitupiana maneno makali kabisa. Inaelezwa kuwa kati ya mambo mengine mengi sababu zilikuwa ni Halmashauri Kuu ya kulivunja Baraza la wazee wa Tanganyika Africa National Union ambao kwa hakika walisaidia wakati wa harakati za uhuru. Hilo lilipingwa na Bibi Titi. Jambo jingine linaelezwa na Mohamed Said katika kitabu chake kuwa Uamuzi wa Bibi Titi kutetea jumuiya ya East African Muslim Welfare Society ambapo Mwalimu Nyerere alipinga hilo kwani aliona ni hatari kuchanganya dini na siasa. Chanzo cha mgogoro wao huo ulionyesha tofauti zao waziwazi nakusabaisha sintofahamu kwa watu wengi.

Wana historia wamejaribu kujua ukweli wa mgogoro huo wa Bibi Titi ili kujua nini kilimsibu mpaka akakosana vibaya sana na wenziwe katika chama cha Tanganyika Africa National Union na kupoteza ubunge na uwaziri, kufukuzwa kama mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Tanganyika Africa National Union, na kupigwa marufuku kwa asasi ya Kiislamu ya East African Muslim Welfare Society ambayo yeye alikuwa kiongozi wake mwandamizi hapa Tanzania.

Anasimulia kijana mdogo Alhaji Abdallah Tambaza; “nikiwa kijana mdogo sana jijini kwetu hapo siku hizo za kudai Uhuru. Kwenye miaka ya mwisho ya hamsini nilikuwa nikimwona bibi yule pale ofisi za Tanganyika Africa National Union ambapo palikua makao makuu, akiwa na viongozi wenzake wakiwa wamesimama nje ya ‘kajumba’ kao kadogo ka Tanganyika Africa National Union ka vyumba sita tu, kalikojengwa kwa miti na kukandikwa udongo. Wakati ule ofisi hiyo ilikua mkabala na shule ya Msingi mnazi mmoja.

“Bibi Titi alikua na binti yake ambaye alikua akija kumtembelea. Nilikuwa nikimwona mitaani kwetu— mtaa wa Sikukuu na Udowe ambako alikuwa akija kumtembelea binti yake peke huyo, Halima aliyekuwa ameolewa hapo na kijana mcheza soka maarufu sana wakati huo Mzee Iddi Hamisi. Mzee Iddi, alikuwa mpachika mabao wa klabu ya Cosmopolitan ya Dar es Salaam, wakati ule klabu hiyo ilipokuwa inawika na kuwa na hadhi kama vile Simba au Yanga kwa sasa. Kwa kweli ilikuwa ndio klabu ya kwanza kupata tiketi ya kuwakilisha nchi kwenye mashindano ya Afrika kwenye miaka ya sitini, lakini ikakwama kutokana na fedha pamoja na uongozi mbovu wa klabu hiyo.

“Lakini mara nyingi nilimfaidi hasa bibi Titi  pale nilipokuwa nikichukuliwa  mimi na ndugu zangu  tukiwa na babetu au mametu, kwenda kwenye mikutano ile ya uamsho na siasa ambayo  Bibi Titi alikuwa mzungumzaji mkubwa, akianza halafu Mheshimiwa Nyerere anamaliza. Kwa zama zile, miongoni mwa Waafrika, mtu aliyepaswa au kustahili kuitwa mheshimiwa, alikuwa ni Nyerere peke yake. Neno hilo ‘mheshimiwa’ hakuitwa Gavana. Ukisema mheshimiwa, hiyo peke yake ilitosha kuwa wewe ulikuwa unaamanisha kipenzi chao Nyerere kutoka Butiama, aliyewashangaza wengi kwa uwezo wake wa kujieleza na kujenga hoja. Ambaye kwa wakati huo, pamoja na sauti yake nyororo na nyembamba, alikuwa akipata taabu sana kutamka neno Watanganyika, ila mpaka kwa kulivuta kidogo Nyerere aliongea kwa madaha na alisifika kwa hilo pia. ‘Wataaa-nganyika wenzangu, Uhuruu na Umoja; Uhuruu na Kazi; Uhuruu na Maendeleo.’ iHyo ni moja ya kaulimbiu kuu za wakati huo.

Kwa upande wa Bibi Titi ni ukweli uliowazi kwamba watu kama akina Bibi Titi hawakuzuka tu na kuwa viongozi katika Chama cha Tanganyika Africa National Union. Watu wa namna ile, wenye vipaji vya namna ile, majasiri namna ile huwa wametengenezwa. Hufundwa majumbani, hupikwa na wazazi wao wakaiva na kuwa tayari kupambana na lolote lijalo katika jamii zao na familia zao. Titi mama yetu ni mmoja wao. Bibi titi mara alipofikia umri wa miaka kumi na mitatu— kwa maana ya ‘kuvunja ungo— tayari alipewa mume. Hiyo maana yake ni kwamba alikuwa tayari amefundwa na wazazi wake mapema kuja kuyakabili maisha na changamoto zake zijazo.

Bibi Titi, akiwa bado kwenye umri mdogo kabisa aliweza kuaminiwa kuongoza katika uimbaji kwenye shughuli za kimila na harusi kwa kutumia sauti yake nyororo, maneno yenye bashasha na vipaji vingi vingine ambavyo alivionyesha tokea mapema. Shneidder Plantan ndiye aliyemwingiza Titi na mumewe katika siasa, baada ya kuwa amependekezwa na wanawake wenziwe waliomjua uwezo wake kutoka katika vikundi mbalimbali vya harakati za kinamama na mambo kama hayo.

Mnamo mwaka elfu moja na mia tisa hamsini na saba, pale kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, mbele ya mgeni kutoka chama cha Labour cha Uingereza, alipewa nafasi kuhutubia mkutano wa Tanganyika Africa National Union wakati Nyerere akiwa Butiama mapumzikoni kwa mamake. Enzi zile kulikuwa na fikra potofu kwamba mwanamke ni mtu wa kukaa nyumbani tu na kulea watoto. Kwamba kazi kama zile za siasa hawaziwezi hata kidogo. Kwa kujiamini na huku akiwaonyoshea kidole wanaume, aliwaambia wanawake wenzake:

“Mnawaona hawa! Basi wafanye watakavyofanya hawa, pamoja na hao wengine wote wanaotisha duniani, wametoka katika matumbo ya wanawake na waliishi humo miezi tisa. Kila mmoja wao kanyonya ziwa la mamake miaka miwili. Sasa tujitokeze wasitushinde hawa!”

“Wanawake amkeni. Tokeni majumbani tuje tupambane pamoja na wanaume mpaka uhuru upatikane. Msiogope. Msiogope. Msiogope!”

“Kutawaliwa siyo kuzuri ndugu zangu. Hili ni letu sote si la wanaume peke yao. Njooni kina dada, njooni kina mama na vikongwe pia!” Alinguruma Titi huku kelele za nderemo, hoihoi na vigelegele vikihanikiza uwanjani pale.

Kwa mara ya kwanza nyimbo zile mashuhuri za kwenye harusi na sherehe nyingine alianza kuwaimbisha wanawake wenzake na kuwatia hamasa isiyo na kifani:

“Hongera mwanangu wee hongera, nami nihongere wee hongera! Mara mbili.

Mama usungu mama usungu! Mara mbili Oieh!

Oieh! Linauma mno wee oieh!

Linauma mno eh! Oieh linauma mno!”

Kutokea hapo siku hiyo, Bibi Titi ikawa ndio habari ya mjini na sifa zake zikazagaa kila pembe ya ukanda huu wa Afrika Mashariki. Wanawake makundi kwa makundi wakawa wamejitokeza na kukikubali chama na harakati zake. Majumbani, kwenye misiba, harusini kote ikawa ndio mazungumzo … Titi…Titi…Titi! Kwa wakati huo wapigania uhuru wa Kenya, akiwamo Tom Mboya, Jaramogi Oginga Odinga (babake Raila Odinga), walipopata habari wakaleta maombi Titi aende kwao kuwasaidia kushawishi serikali ya Muingereza kumtoa kifungoni Mzee Jomo Kenyatta— babake Rais Kenyatta aliyestaafu mwaka huu— kwa kosa la uhaini wa kudai kujitawala.

Bibi Titi alitia fora kwenye mikutano yake kule Mombasa, Kisumu, Machakos na Nairobi. Titi, alisimama majukwani kule Kenya akiwa amevalia ‘mini skirts’ zake maridadi kabisa, akilia kwa uchungu kumpigania Kenyatta awe huru na wanawake waje wajae kwenye harakati. Haikupita kitanbo sana, miaka kadhaa baadaye, Mzee Jomo Kenyatta aliachiwa huru kule Kenya na haraka haraka akaja Tanganyika na kuhutubia maelfu ya watu—akiwemo mwandishi huyu— pale kwenye viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.

Kenyatta akiwa amevalia suruali yake ya corduroy rangi ya udongo maarufu khaki Kenya siku zile na koti kubwa la kijivujivu. Alipeperusha juu usinga wake mweusi na kutumia muda mwingi kumshukuru Bibi Titi kwa kazi aliyowafanyia Wakenya. Kwenye mkutano ule ndipo Nyerere alipotamka kwamba yuko tayari kuahirisha uhuru wa Tanganyika ambao tayari ulikuwa umeshajulikana, ili tusubiri Kenya nao wapate wa kwao na hapo nchi hizi ziungane kuwa moja na Kenyatta awe ndio rais wake. Ni tamko zito sana hilo, ambalo bila shaka yeyote lilitokana na kazi ya Mama Titi. Uhuru uchelewe na urais apewe mtu mwengine! Leo isingewezekana. Si unaona Zanzibar? Karume kataka mwenyewe Muungano haraka kwa kuogopa kupinduliwa, leo inaonekana kalazimishwa na Nyerere.

Baada ya Uhuru kupatikana, Bibi Titi alipata ubunge jimbo la Rufiji, na akachaguliwa kuwa Waziri Mdogo wa Wizara ya Utamaduni na Maendeleo. Alikuwa pia mweyekiti wa mwanzo wa Umoja wa Wanawake Tanzania na kiongozi mwanadamizi wa East African Muslim Welfare Society tawi la Tanganyika, pamoja na mjumbe wa Maulid Committee kamati ndogo ya kuandaa Maulid kila mwaka. Mwenyekiti hapo akiwa waziri mwenzake Tewa Said Tewa, Mbunge wa Kisarawe na Chifu Abdallah Said Fundikira aliyepata kuwa Waziri wa Sheria akawa Katibu kwa wakati huo.

Timu hiyo kwa kushirikiana na wajumbe wengine hapa nchini walifanya mambo makubwa sana katika kuendeleza maisha ya wana jamii, na kwa kiasi fulani walifanikiwa katika kutaka kupunguza pengo lililopo kielimu baina ya Waislamu na watu wa dini nyengine. Mara ghafla walifanikiwa waliweza kupata kiwanja kikubwa pale Chang’ombe karibu na Uwanja wa Taifa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha kwanza Tanganyika, kabla hata kile cha Mlimani hakijaanza.

Bibi Titi na wenzake kumwalika Nyerere kuja kuweka jiwe la msingi, Nyerere na serikali anayoiongoza, inasemekana hakupendezwa na jambo lile. Mipango ikafanywa, si tu kuusimamisha mradi ule uliokuwa unafadhiliwa na Rais wa Misri wakati huo, Gamal Abdel Nasser, bali kuivunja kabisa taasisi ile ya East African Muslim Welfare Society na kuwaundia Waislamu baraza jengine. Mwalimu na wenzake katika Tanganyika Africa National Union , pamoja na kukataa ubaguzi kwa kukubali kuwapokea na kuwapigia kura Wahindi kwenye mpango wa ‘kura tatu’, kwenye hili la Uislamu Wahindi wakaonekana. Wahindi  hawakutakiwa wasaidie Waislamu wenzao na hapo ikavunjwa East African Muslim Welfare Society  kwa amri ya Serikali na likaundwa Baraza kuu la Waislamu Tanzania ambalo lilikua la  Waafrika watupu.

Bibi Titi alipoteza kiti chake cha ubunge Rufiji kwa mtu aliyekuwa si maarufu hata kidogo. Tewa naye alipoteza Kisarawe na alipelekwa kuwa Balozi wa Tanzania kule China. Alhaji Chifu Abdallah Said Fundikira akapelekwa Nairobi, Kenya kuwa Mwenyekiti wa ‘marehemu’ Shirika la Ndege la Jumuiya Afrika Mashariki lililouawa kikatili Juni thelathini,mwaka elfu moja mia tisa sabini na saba. Ndani ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Tanganyika Africa National Union, hayati Bibi Titi alipambana na kuwagaragaza wanasiasa wakongwe kwa hoja nzito pale mjadala wa kuivunja EAMWS ulipokuwa unajadiliwa na halmashauri hiyo.

Bibi Titi mwenyewe, miaka thelathini baada ya kuangushwa kwake kisiasa ameliambia gazeti la Rai kwamba kuanguka kwake kisiasa kulisababishwa na kule kumpinga Nyerere kwenye Halmashauri Kuu ya  Tanganyika Africa National Union, wakati Nyerere alipokuwa anatafuta kuungwa mkono na Waislamu ndani ya chama kwa kuivunja East African Muslim Welfare Society. Mnamo mwaka elfu moja na mia tisa  na sitini na nane, Bibi Titi alikamatwa pamoja na mwanasiasa mwengine aliyepata kuwa Waziri wa Kazi na kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi nchini Michael Kamaliza, kwamba walishirikiana na wanajeshi wengine wanne wakitaka kumuua na kuipindua serikali ya Nyerere. Bibi Titi na wenzake walitiwa hatiani katika kesi iliyochukuwa siku mia na ishirini kusikilizwa, na hivyo kufungwa jela  kifungo cha maisha.

Wahenga wana msemo usemao tenda wema nenda zako. Habari za kukamatwa na kufungwa jela kwa Bibi Titi ziliwashitua na kuwasikitisha mno watu wa Kenya, na hasa wanawake ambao walikuwa wana deni kwake.Mwanamama mmoja, mwanasiasa machachari nchini Kenya, alivuka mpaka na kumfuata Nyerere Butiama alikokuwa amepumzika nyumbani kwao baada ya kuomba wakutane huko mbele ya mamake Mwalimu, Mama Mgaya. Baada ya mapokezi na maamkizi, mama yule alimkabili Nyerere uso kwa uso na kumwambia kuwa alichofanya ni kukosa fadhila kwa Bibi Titi ambaye amewafanyia makubwa watu wa Afrika Mashariki ujanani kwake sio tu kwa watanganyika bali hata wakenya.

“Utakuwa ni wizi wa fadhila na kukosa utu kama wewe Nyerere utaendelea kumfunga jela Bibi Titi kwa yote aliyokufanyia wewe, nchi yako na wapenda haki na usawa wote wa upande huu wa dunia. Tafadhali sana nakuomba nimetumwa kwako nikiwakilisha watu wa Kenya na wanawake wa nchi hizi mbili umwachie huru Bibi Titi, kama yeye alivyopambana na Wazungu mpaka Kenyatta wa kwetu Kenya akatoka jela.”

Alipomaliza mazungumzo hayo mama yule akarudi kwao Kenya.

Siku moja mama huyo akiwa ofisini kwake Kenya tayari ameshasahau; mara akapata habari kwamba kuna mgeni kutoka Tanzania anataka kumwona. Akaagiza apitishwe. Alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje John Samuel Malecela akiwa na ujumbe kutoka kwa Mwalimu.

“Nimetumwa nije nikupe habari njema kwamba Nyerere tayari ameshamwacha huru Bibi Titi,” alisema Waziri Malecela. Mama alijibu, “Kamwambie Nyerere kwamba kwa niaba ya wanawake wa Kenya na watu wa Afrika Mashariki, ninasema ahsante sana kwa uungwana wake.” Alimaliza kwa kusema hivyo. Mzee Malecela alirudi Tanganyika.

Baada ya hapo, Bibi Titi aliishi maisha ya upweke bila ya familia yake wala marifiki zake aliokutana nao wakati wa harakati zake za kisiasa. Mme wake, Boi Selemani pia alimwacha na jamii yote ilimtenga. Hivyo ndivyo alivyoishi baada ya kufunguliwa mama yetu. Aliyerejea tena kuishi maisha ya chini kabisa ya kawaida kule Temeke, mtaa wa Ngarambe, maana nyumba zake mbili za kisasa pale Upanga alizokuwa akimiliki wakati wa enzi zake za uongozi zilitaifishwa na Azimio la Arusha. Aliwekwa chini ya ulinzi fulani hivi hakua na uhuru wa kwenda alipotaka, maana kutwa alikuwa akikaa nje barazani kwake akiiuza mafuta ya taa kwa kupimia watu rejareja na siku zikawa zinasogea mbele, maisha yale ya umaarufu na kujiweza kiuchumi yakawa ni ndoto kwake.

Baada ya kutengana na Julius Nyerere ikawa vigumu kupata taarifa zozote zinazomhusu Bibi Titi Mohamed. Kwa muda mrefu, serikali ilikaa kimya kuhusu mchango wake na mafanikio yake. Ukosefu huu wa kuutambua mchango wa Bibi Titi Mohamed katika harakati za ukombozi wa Tanganyika unaendana na tabia iliyozoeleka ya kutotambua michango ya wanawake, hasa ya kisiasa inayoandikwa katika vitabu vya historia.

Lakini Rais Mwinyi alipokuja madarakani alimrejeshea mama yule zile nyumba zake mbili pale Upanga, na habari zinasema akapewa na senti mbili tatu kujiendesha maisha yake yaliyobaki. Ila hakuweza kurudi kwenye majukwaa tena na kuendelea kupigania haki za wanawake na kuleta mapinduzi ya kifikra kwa jamii yake hasa wanawake, lakini mambo yalibadilika elfu moja mia tisa tisini na moja. Katika chapisho la chama la kuadhimisha miaka thelathini ya uhuru, Bibi Titi alitajwa kama “shujaa wa kike katika harakati za ukombozi”. Moja ya barabara kuu jijini Dar es Salaam imepewa jina lake. Bibi Titi alifariki dunia mnamo mwaka elfu mbili. Watanzania wengi wanamkumbuka kama “Mama wa Taifa”. Tunamwomba Mola ailaze mahala pema peponi roho ya mama yetu huyu.

Hivyo ndivyo historia ya Bibi Titi ilivyosimuliwa na mmoja kati ya watu waliomuona katika harakati zake za kuikomboa nchi yake hususani kukomboa fikra za wanawake, lakini pia hata kusaidia nchi zingine kupigania haki zao. Bibi Titi kweli alikua mama wa taifa lakini pia shujaa wa nguvu npambanaji, mfano wa kuigwa kaitika jamii zetu leo zilizo kandamizi dhidi ya wanawake katika nyanja zote kichumi, kisiasa na hata kijamii mwanamke hana dhamani na ni kiumbe dhaifu, kisicho stahili nafasi yoyote. Dhana hizi potofu lazima tuzipinge kama wana jamii ili kuinua uchumi wa nchi lakini pia kukomboa jamii zenye tamaduni kandamizi dhidi ya wanawake.

Image credit

 

Common Voice, kenya, kiswahili, Mozilla, Mwalimu Julius Nyerere, Tanganyika, Zanzibar


Hekaya Initiative

Writing the East African Coast.

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

© Hekaya Initiative 2018-2020. All Rights Reserved. Design by Crablinks
%d bloggers like this: