Washindi wa awamu ya pili ya mashindano ya uandishi

Baada ya majumaa kadhaa ya kupitia kazi zilizowasilishwa kwenye awamu ya pili ya haya mashindano, washindi wameteuliwa. Kama tulivyotaja hapo awali katika awamu ya kwanza, kazi tunazozipokea kwa lugha ya Kiswahili ni nzuri kiasi cha kwamba kama nafasi ingepatikana, tungeandaa warsha ya uandishi ili kukuza vipaji zaidi na kuzalisha kazi nyingi tu kwa lugha hii yetu adhimu.

Warsha kama hii kwa kiasi kikubwa itawawezesha waandishi kuandika kazi imara zaidi ambazo zinaweza wasilishwa kwa wachapishaji na pia mashindano mbalimbali kama vile Tuzo ya Safal-Cornell. Kazi ikiwa nzuri itafungua milango ya kufasiriwa kupelekwa lugha zingine. Hapa pia mwandishi atafahamu zaidi namna ya kufanya riwaya itiririke vizuri, kisa kuleweka, kuzingatia hadhira na sana sana wahusika kujengeka kwa ustadi.

Washindi kutoka nambari tatu hadi moja ni kama hivi:

3. Bibi Titi- Rahma Mkai

Hii ni kazi inayoelezea historia ya Marehemu Bibi Titi Mohammed, mwanamke aliyechangia katika harakati za ukombozi Tanzania na mataifa jirani, japo hakutambuliwa na kupata heshima aliyostahili. Ni makala yanayoelimisha na kumshurutisha msomaji kujiuliza maswali zaidi, ikizingatiwa kwa kiasi kikubwa, bado nafasi ya mwanamke haijatambuliwa kikamilifu, na ukandamizaji unaendelea. Ni rahisi kutambua na kufurahia kuwa aidha mwandishi alifanya utafiti inavyohitajika, au historia hii iko kwenye kitanga cha mkono wake

 

2. Chini Ya Mvungu- Lilian Mbaga

Kwa lugha tamu mwandishi anazungumzia maswala ya siasa/demokrasia/ukoloni mambo leo, akisaili ni nani atachukua jukumu la kumkomboa sisimizi (Mwananchi/Mwafrika) kutoka kwa mikono ya Wa Ahadi (wanasiasa wanaowakandamiza)

Riwaya pia inaeleza changamoto na misukosuko ambayo wanaharakati wa kisiasa wanokimbilia ughaibuni wanakumbana nayo.

1. Malkia Aishi Milele- Hassan Kassim

Hii ni kazi inayogusia maswala mbali mbali ya kimataifa kama vile ukoloni, demokrasia, vita vya
dunia na kadhalika. Mwandishi ametumia lugha ya kuvutia, na kwa urahisi sana inamwalika
msomaji katika dunia ya kujadili falsafa. Anaonyesha uelewa wa maswala mengi ya kihistoria na
bila shaka atapongezwa kwa utafiti aliofanya kwa ajili ya kazi hii.

Hongera kwa washindi wetu watatu na hongera kwa wote walioshiriki. Kama ambavyo tushataja hapo awali katika awamu ya kwanza ya haya mashindano, kazi zinazowasilishwa kwa Kiswahili ni nzuri sana kiasi kwamba ata kuteua mshindi yawa kibarua kizito, maana kazi zote ni maridadi sana.

Shukrani zetu kwa shirika la Mozilla Foundation kwa kuwezesha uwepo wa shindano kama hili. Yapendeza sana mara waandishi wa Kiswahili wanpaata kuzawadiwa kwa kazi zao. Tungependa kuhimiza kila mtu kutembelea tovuti yao ya Common Voice ili kujisajili na kuchangia ima sauti au sentensi ili tukuze Kiswahili kama lugha ya mashine.

Tutaanza kuchapisha kazi za washindi hapa kwenye tovuti yeti kuanzia kesho.

 

Common Voice, kiswahili, Mozilla, Mozilla Foundation


Hekaya Initiative

Writing the East African Coast.

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

© Hekaya Initiative 2018-2020. All Rights Reserved. Design by Crablinks
%d bloggers like this: