Chini Ya Mvungu

imeandikwa na Lilian Mbaga

“Hata mkilia haitasaidia,” alisema sisimizi mwenye kichwa kidogo.

Sisimizi mwenye mtoto mgongoni aliyekuwa ndani ya masurupwete akaongeza, “Wametudanganya – wametudanganya hawa.”

Kwa pamoja vinywa vyao vikatoa sauti dhaifu iliyokosa matumaini, kwa unyong’ofu na simanzi kubwa wakatamka, “Wa ahadi tangu tulipowaona kipindi cha mitano nyuma – ’ Wakameza mate kwa midomo yao midogo iliyopauka kwa kiu, Sura zao zilichoka kwa dhiki na mashaka makubwa kisha wakaendelea, “Hatujawaona tena – wa ahadi wametusahau.”

Kimya kikatanda. Kila sisimizi akazama fikrani bila kuzingatia udogo wa kichwa chake na kuchambua yote kwa kina. Fikra zao zilifanana: dhiki, ufukara na ugumu wa kumudu gharama za maisha.

“Tutawaona lini?” Sisimizi jabari akahoji kwa ghaidhi iliyojaa uchungu.

Wakatazamana kwa hofu. Si kwamba sisimizi walikuwa bongolala, la hasha! Fikra zao zilipuuzwa. Ijapokuwa vinywa vyao vilijawa na kitete kukiri, yamkini walijua ni lini watawaona tena wa ahadi: kuwaona baaada ya nusu mwongo. Wakabebetua midomo yao huku wakienda yosi kwa matumaini huenda wa ahadi watarudi kabla ya miaka mitano kufika.

Wa Ahadi, sifa yao kuu ni kunyenyekewa na kusifiwa hata pasipo hitajika kufanywa hivyo: wapambwe kwa mapambo ya sifa kemkemu ambayo aghalabu hawastahili: iwe kwenye vyombo vya habari au majukwaani, na kinyume chake hufoka kwa cheche za vitendo: kufungia vyombo vya habari vilivyofichua uozo wao au kupigwa faini ndefu ya kufilisi, au kuamrishwa kuomba radhi kwa ukweli ulioibuliwa.

Wa ahadi wana ndimi tatu; ya kwanza kutoa ahadi kabla ya mitano; ya pili kutumia kinywa kwa umahiri kama wao sio wawakilishi wa sisimizi, na kupoteza kusudi la uwepo wao. Ya mwisho, Kubadilisha nyeupe – kuwa – nyeusi na nyeusi kuwa nyeusi zaidi! Au rangi yoyote itakayoendana na azma yao na matamanio ya ulafi wao.

Wa ahadi sijui wao hupata elimu wapi! Kwa Sababu chuo wanachosoma hutoa zao la wachunga wenye talanta kubwa, ni kama wote hufanana matendo yao, hata wale waliokuwa na insafu njema awali, hujigeuza rangi zao kwa kuwa vinyonga vile ilivyowafaa: walipokaa na sisimizi walikuwa na rangi nyeupe, walipokuwa ndani ya mhimili mkuu kuwakilisha sisimizi rangi ilibadilika kabisa, na walipokuwa mafichoni rangi zao ziligeuka mithili ya gamba la chatu. Ewe sisimizi kuwa makini!

Ajabu ni kwamba kila kiumbe kina kina ajabu zake: wa ahadi hawajahi tambua ajabu zao abadani! Ipo hivi: Wa ‘ahadi’ kama ada yao hutoa maneno matamu yaliyosheheni ahadi kemkem, kwa kauli laghai ‘sisimizi’ huamini kila neno: bila kujua kwamba kwamba ni mtego wa kunasa! Aghalabu ajabu zao hupendwa na baadhi ya sisimizi.

Iligeuka ada kwa wa ahadi kuonekana kila baada ya nusu muongo na kutengeneza usuhuba wa kujikomba kwa sisimizi, na kutoa ahadi nyingi zenye idadi lukuki ijapokuwa hazitimiliki. Baada ya hapo hawaonekani tena machoni mwa sisimizi, na kuishia kuwaona kwenye televisheni tu: namna wanavyosinzia na kupitisha hoja dhaifu na wanavyopitisha bajeti zenye kumdidimiza sisimizi.

Gizani au ndani ya nuru – hadharani au kifichoni: sisimizi walihofu kuhusu hatima yao. Kwa jadi ya haiba ya uraufu wao na udogo wa vinywa vyao, uoga wa kutokuwa na mamlaka ukawadogodisha mara elfu, hata wawe vipofu – wasione matendo ya wa ahadi, wakawa mabubu na viziwi kujifanya hawasikii nyimbo za wa ahadi.

“Wamerudi – wamerudi,” Sisimizi mwenye tumbo kubwa alisema kwa sauti ya kuwashtua wenzake. Kwa pamoja wakakumbwa na butwaa.

Wakahesabu vidole vya mikono yao, moja, mbili, tatu, nne na hatimaye kukamilisha ngumi ya mkono ‘tano’ chaguzi mlangoni. Wanarudi leo? Wakahojiana wao kwa wao pasi jawabu, Walikuwa wapi? Wamerudi kufanya nini? Hawaoni haya? Ndani ya nyoyo zao walijua fika wa ahadi wamerudi kwa maslahi yao na sio maslahi ya sisimizi.

Sisimizi walipogundua hila zao wa ahadi, wakagutuka ndani ya dimbwi la njozi mbaya.  Kama ilivyo jadi yao wakaungana kwa umoja wao na kufuatana kwa msafara, wakadhibiti sisimizi wenzao kwenda arijojo – mguu kwa mguu. Loh! Hawakufanikiwa. Safari yao ikakumbwa na misukosuko – wakasombwa kwa kushindwa kuhimili gharika la jazba ya mamlaka. Wengine walijeruhiwa kutokana na udogo wao huku wengine wakikumbwa na umauti huku wakikosa kushuhudia hatima ya safari yao.

Baadhi ya sisimizi wachache waliobahatika kubaki hawakuwa hai – wala maiti kwa kihoro. Kila walipokumbuka yaliyowakumba jamaa zao – wakatia vinywa vyao gundi.

Baadhi ya sisimizi na wa ahadi hujitahidi kutetea kwamba, “Majanga yote yamesababishwa na wakoloni wale waliokuwepo barani kote Afrika kupata malighafi.”

Ijapokuwa, hoja hiyo ilipata mashaka kutoka kwa sisimizi mwerevu, ambaye mpaka sasa haijulikani alipo hata baada ya vyombo vya dola kumtafuta. Alipotea mithili ya kipini mchangani. Vilio vya jamaa zake havikusaidia kumrudisha. Kwa fununu tu ni kwamba aliangamia mikononi mwa wa ahadi.

Na haya ni maneno yake yaliyopata kunukuliwa:

Wale – wezi wa ‘Malighafi’ ambao hupenda kuwataja kwa majina yote mabaya kama ‘wakoloni, na mabeberu’, walishaondoka yapata miongo mingi sana. Na ubaya wa athari zao zipo dhahiri na wala sikatai walituachia athari hasi: umaskini, maumivu, chuki, lakini kwa nini hadi sasa tuwalaumu? Kwamba wao ndio sababu ya sisi kuwa hivi? Wao ndio sababu ya sisimizi kuumia mpaka sasa? Wao ndio sababu ya sisimizi kukosa huduma ya matibabu bora? Wao ndio sababu ya wanafunzi kukosa madawati? Wao ndio Sababu ya sisimizi kukosa milo mitatu kwa siku? Wao ndio sababu ya barabara mbovu? Wao ndio sababu ya sisimizi kukosa uhuru wa kujieleza? Wao ndio sababu ya sisimizi kuwa wajinga? Wao ndio sababu ya ‘wa ahadi’ kung’anga’nia kuketi miaka mingi madarakani? na walipobanduka basi kuwaachia makinda yao?

Akamalizia kwa kusema, “Wa ahadi wametufikisha hapa.”

Wa ahadi hana haja ya kujitambulisha kwamba yeye ni wa kutoka koo hiyo. Utamtambua kwa matamshi yake pale anapofungua kinywa chake. Wengine wanaonekana kwenye sehemu iliyofanywa ulimwengu kuwa kijiji huko; wakijitapa kwa vitendo bila kutamka ‘hapa najitapa’ wakitoa vitisho kwa sisimizi wachokonozi kwenye mada zilizobeba misamiati migumu. Wa ahadi hufanya vile atakavyo na kwake yeye huona ni hisani kwa yale anayopaswa kutenda kwa sisimizi. Kwao wajibu ni hisani.

Sisimizi waliojaribu kuweka wazi fikra za uono wao juu ya matumizi ya pesa za jumuiya ya sisimizi wenzao, wakaambiwa wao si wazalendo, na lengo lao ni kuleta machafuko na kuzua taharuki. Na wale – wa ahadi waliokamatwa kwa ufujaji na ubadhilifu, ripoti zao zikatolewa, wakaendelea kuwa huru mtaani na kutumia kodi za sisimizi. Nani wa kuwagusa? Sisimizi huyu huyu mwenye kaumbo kadogo mithili ya kiroboto? Anha – wapi!

Kuna wale sisimizi wenye uthubutu haswa, Naam! Wakajaribu kujiunga kwa umoja wao na kutembea kwa msururu maili elfu. Vichwa vyao vilijitwika mabango yaliyosheheni manun’guniko yenye ukweli mchungu. Wa ahadi hufanya mambo mawili, hufunika ukweli mchungu kwa uongo mtamu au kutojali asilani. Au kuwatawanya sisimizi kwa virungu na silaha ya bomu la machozi.  Wale wale sisimizi waliopewa ahadi tamu wakatolewa mbio kwa king’ora hata kusikilizwa tu hakukuwepo! Ni kama wana ka’ugonjwa ka’kusahau vibaya. Wa ahadi yupo kwa ajili ya nani? Kumwakilisha nani? Hili si fumbo tata endapo humwakilisha sisimizi.

Wapo sisimizi waliothubutu kujipa vichwa vikubwa! Wakajaribu kuwa mwewe, kwa kupaa na kusambaza habari kwa sisimizi kuhusu hila za baadhi wa ahadi, na taarifa zao zenye mashaka. Loh! Hawakudumu, kwani cheche za moto ziliwafikia huko juu walipokuwa. Wakawa kunguru waoga waliochagua sehemu ya kurukia na kutua. Ijapokuwa walijitahidi, kusimama tena lakini walizidiwa nguvu. Wakakimbiza mbawa zao ughaibuni, wakabaki na harakati zao huko huko, kwako na kwa majirani zako wapo! Tazama kwa makini tu, utawajua! Lakini ukweli mchungu ni kwamba makucha yao hayana ukali ule wa mwanzo. Lenye kutia simanzi huonekana ni wasaliti ambao husemwa, ‘Wanatumiwa na mabeberu hao.’

Hata wale sisimizi waliojaribu kuwa kama mwewe wakatolewa maneno ya cheche zilizotoka kwa ghadhabu, ‘Uthubutu huo umetoa wapi ewe sisimizi? Nani aliyekuvisha mbawa na kupiga kelele kama umeona mzoga?’

Sisimizi wakadhofishwa kwa cheche za ghadhabu na hadaa ya maneno ya wa ahadi yaliyotoka vinywani mwao. Wakajaribu kukimbiza mbawa zao mithili ya kunguru mwoga hufanya, la! Wengine walidhoofu hata kushindwa kurusha mbawa zao: cheche zikawaacha na vilema vya maisha, macho yakatobolewa, ndimi zikanyofolewa na wasipate kunena tena! na wengine kupewa kesi zisizoweza kuwatoa korokoroni. Kwa kuona hilo sisimizi wengine wakawagofya na kujiweka kando.

Udogo wa sisimizi si hoja ila ni umoja wao, ijapokuwa wameshindwa kuwa kitu kimoja. Ingawaje, sisimizi hawa hawa wakasema, ‘Eti aliye kando haangukiwi na mti,’ Asalale! Huu ni uongo! Uongo wa kujipa moyo kwamba wapo salama. Unawezaje kukaa kando kwa kusema siasa zao hazikuhusu? Hujui kama kila kitu kinaathirwa na siasa zao? Ukinunua shati mtumbani, ukinunua chupa ya maji au kulipa bili ya maji, ukinunua sukari, ukinunua chakula, ukitumia usafiri. Sisimizi, huwezi kukaa kando kwa likuhusulo! La sivyo utaendelea kufanyiwa maamuzi kwa kila kitu kwa fedha yako mwenyewe.

Afrika kipi kinachokusibu? Umekosa nini Afrika? Kupinduana wenyewe kwa wenyewe! Mapinduzi ya kijeshi na utawala wa kijeshi. Juzi tu Afrika Magharibi tumeshuhudia. Mmewahi kuwafikiria sisimizi? kwa utulivu wao na maumivu mnayowapelekea? Ni kweli Afrika kichwa cha mwendawazimu?

Wa ahadi ni mithili ya papa wa nchi kavu, kuonekana kwao ni kila baada ya mitano. Sisimizi hawajui wapeleke wapi changamoto zao, au kufuatilia ahadi walizoahidiwa kwamba zitatimizwa ndani ya muda wao wa uongozi.  Wakaendelea kuteseka na matatizo yao wala wasiomuone yule aliyejinadi kwamba yeye ndio mwokozi na mtatuzi wa kila gumu lihusulo hatma ya maisha yao.

Ni juzi juzi tu hapa, vigoma vikachezwa – kwa mlio mkubwa – ngoma zikatoa mlio, ‘ndu ndu ndu!’ Huku sisimizi wakiyapamba mashairi yaliyo finyangwafinyangwa kwa ustadi wa ndimi zao: Wa ahadi siku zote hutumia sisimizi kitengo cha sanaa kuvutia sisimzi wenzao. Nao hupata fedha, basi husifia hata visvyostahili kupata sifa, mashairi yao hujaa uongo uliopaswa kusemwa ukweli, hupindisha yale yaliyopaswa – kunyooshwa. Pasipo soni, huwashawishi sisimizi wenzao na kuaminika kwa wengi wao. Ati kwamba msanii ni kioo cha jamii haipo tena, Loh! Kwao ni msanii mchumia tumbo, fedha mbele.

Kwa mashairi hayo ya sisimizi wasanii basi, Ka’mtaa kakafurika hadi kufunga. Wa ahadi akapanda jukwaani, safari hii akaimba ngonjera zile zile kama za mitano ya nyuma.  Kinywa chake kikatoa cheche za upole. Si kuna msemo kwamba: mikono mitupu hailambwi? Akafungasha vijizawadi akafungasha – Khanga, fulana na kofia. Ewe sisimizi zawadi hizo ndio umeona za muhimu? Mpaka uso wako ukajawa bashasha na kutabasamu huku meno thelathini na mbili nje! Sisimizi wakashukuru kana kwamba ni johari kwao kupata matibabu bora, kuongeza zahanati, elimu bora au kupunguza ukali wa maisha. Afrika, Afrika! Kweli zawadi ya kanga? Na kofia ndio iwe mtego wa kunasa? Umpe wa ahadikula’ yako kwa sababu ya burudani iliyokonga moyo wako? Au uchague sera dhidi ya zawadi.

Sisimizi wenye msimamo wakaishia kusema heri ya mrama kuliko kuzama, na mikono yao nyuma wakaiweka mbele hawakuinyosha kupokea vijizawadi. Wakapuuza ahadi hewa zilizopambwa kwa maneno matamu yenye kutoa udenda wa matamanio. Sisimizi, sisimizi – nawaita kwa mbiu ya mgambo! Ina maana hamuoni? Hamuoni kama mnachezewa? Kwa nyimbo zile zile kila ikaribiapo miaka mitano?

Amani! Amani! Ndio wimbo wa ahadi. Kila sisimizi wanapojaribu kufurukuta na kuwa wamoja basi wa ahadi hutoka vifua mbele na mabavu ambayo bila jicho la tatu ni ngumu kuyaona. Kwa sauti ya mabavu husema, “Amani yetu tuliyoitunza kwa miaka mingi, msiruhusu vikundi vya watu wachache waipoteze, kamwe!” Mbinu yao ya kukimbia majadiliano huwa ni kigezo cha amani. Hulka ya sisimizi yao ni upole, aghalabu basi hurudi nyuma kwa hofu.

Wa ahadi wao hujenga madaraja ya matumaini – nao sisimizi huamini kila kiumbwacho kinywani mwa wa ahadi. Utawasikia wakisemazana wao kwa wao, ‘Wa ahadi kasema barabara itajengwa, hivyo tutapita kwa raha mustarehe.’ Hamjui, hamju nakuambieni! Wa ahadi ni janja janja sana, basi wakiahidi daraja imara basi watayavunja matumaini hayo, nao watapiga mbizi. Hamjui ni mahiri wa kuogelea kama ambavyo huogelea ndani ya akili na fikra zenu? Na wakifanikisha kuvuka ng’ambo basi hubakia kuwatazama kwa mbali na kuwapungia mikono yao hewani.

Kwa dhahiri tunaona mambo kede wa kede kwa majirani: wale walioweka gundi kwenye viti vyao kila wakiinuka basi wanainuka na viti vyao, kwao madaraka yamegeuka mimba zisizotarajiwa kujifungua. Hata mazao ya mayai yao waliyotaga humo wanataka yabaki hapo, wanakuwa wakali endapo sisimizi atajaribu kuyatoa. Kuna haja ya kuwataja? Wapo wale wa kihistoria hata wa sasa hivi. Sisimizi yeyote anayejaribu kuwatoa kwenye viota vyao basi cheche kubwa na nene zenye makali huwakumba. Kwanza, hufungwa vinywa vyao milele, na endapo wakabahatika kuvuta pumzi basi huwa ahueni kwao: na pumzi wataivutia korokoroni.

‘Nyau nyau nyau’ sauti ya sisimizi pale anapojaribu kujivika mabavu. Wa ahadi aogope sauti ya paka? Umewahi kuona wapi? Hata wakikunjua makucha yao – kucha zao hukatwa kwa mapanga, visu, nyundo. Kwao husema vita haina macho – zana yoyote hutumika. Na hapo sisimizi wanakuwa butu! Wanarudi kuwa na umbile lao la siku zote.

Ni ulafi – ulafi mkubwa kabisa umejaa matumbo yao na nyoyo zao – zimejaa maradhi. Nyoyo zenye maradhi – hasara tena hasara kubwa. Loh! Wa ahadi kwao hilo hawajali. Iangalie Afrika yote – kwako – kwangu na kwao – jiulize swali hili sisimizi ni fukara kiasi hiki? Wa ahadi kwa nini wakose vipaumbele? Au waende tu mithili ya ngoma ya ngoma ya mwendawazimu? Hawaoni au hawajui sisimizi wanahitaji kipi?

Wa ahadi akishikwa na homa ya ghafla hukwea pipa ughaibuni kuchomwa sindano! Afanaleki! Aibu kubwa. Hii pia wa mabeberu wametusababishia? Kipi kinafanya wasijenge zahanati, hospitali kubwa zenye kutibu maradhi yote makubwa makubwa.

Haitoshi, huendelea kusema elimu yetu ni bora kuliko ukanda wowote wa Afrika! Kweli? Watoto wakirudi nyumbani sare za shule zimechafuka kwa vumbi, mathalani walienda shamba kumbe kusoma. Ndio! Madawati haba, hadi zama hizi ni sahihi kupigania kuhusu mbao za kukalia?

Enhe! wa ahadi utasikia wakisema huku wamezungukwa na vipaza sauti “Lengo letu kubwa ni kupata wanasayansi.” Kichekesho, watoke wapi wapi kwa juhudi gani walizowekeza? Maabara hakuna na zilizopo hazitoshi. Vitendea kazi ni sifuri jumlisha kumi kati ya sisimizi mia. Uwiano upo wapi? Makinda yao wameyapeleka nje kupata neema.

‘Kuna ubadhilifu wa pesa mkubwa umefanywa na wa ahadi’ basi utakuta sisimizi vijiweni wamejitenga wakisimuliana, ‘Atafungwa yule.’ Wafungwe wapi? Yaani una maanisha wa ahadi ndio wafungwe kwa mfumo walioujuenga kwa mikono yao wenyewe? Hamjui kama wana umoja wa kulindana?

Sisimizi mmoja mjuzi wa mashairi akaimba ka’wimbo kake. ‘Afrika, Afrika ni nini wataka Afrika? Afrika Afrika nikupe nini Afrika? Sisimizi wengine wakabadilisha mashairi yale wakaimba, ‘Huna cha kuipa Afrika, wa ahadi wana tuangusha Afrika?’ Nyimbo za sisimizi na wa ahadi tofauti yake ni – uchezaji wao, tofauti – wao wanacheza ili kukonga nyoyo zao. Sisimizi wao uchezaji wao ni rahisi sana – kupata maji salama, elimu bora, malazi na chakula. Ni rahisi enhe?

Sisimizi wanahitaji huduma ya afya bora, wakifika kituo cha afya kwa maradhi yao basi wapate huduma wanayostahili. Wapate vipimo, dawa za uhakika. Wajawazito wanapojifungua basi wapate huduma bora na salama kwa mama na mtoto. Watoto wao wakienda shule wapate elimu iliyo bora yenye maarifa kwao: Ikiwamo upatikanaji wa vitabu vya kutosha, maabara na nyenzo za kujifunzia. Wanahitaji miundombinu rafiki, ili wasafirishe mazao yao kuweza kufanya biashara zao. Wanahitaji kuishi maisha yaliyo juu ya mstari wa umasikini, na sio kinyume chake.

Nani aliyewaambia wa ahadi kujilipa mishahara mikubwa mikubwa na marupurupu kibao? Tena kwa kodi za sisimizi. Wakijitunuku vyeo na majina makubwa huku wakijitia kuwa wapo juu ya sheria. Huku sisimizi walimu, watabibu na askari polisi wakilipwa kiasi kidogo tu ambacho asilimia kubwa huishia kwenye kodi na gharama nyingine za maisha. Wanasisitiza sisimizi kujiajiri huku mazingira si rafiki, wana sisitiza sisimizi kutochagua kazi huku wao wakin’gan’gania viti walivyokalia. Na wao kuishi mithili ya wafalme kama vile wapo nchi ya ahadi! Hawaijui njaa wala nini maana ya kukosa huduma muhimu.

Nani atainama chini ya mvungu na kuwatoa wa ahadi wa Afrika waliojawa rui na kuwaweka juu ya godoro kisha kulimwagia maji ili wasipate usingizi? Ni lini sisimizi wa Afrika wataamka na kuwatoa wa ahadi chini ya mvungu na kuchukua hatua kali dhidi yao? Ni lini sisimizi wa Afrika wataamka na kufanya gwaride la usafi kwa kutoa takataka, uozo wa ubadhilifu wa fedha za umma, uzembe, mikataba hewa ya madini na miradi.

Ni lini sasa sisimizi watasema, ‘Sasa inatosha!’ Oh! sisimizi wa Afrika, nani yupo tayari kuinama chini ya mvungu?

Picha

 

 

 

 

 

Africa, kiswahili, Mozilla


Hekaya Initiative

Writing the East African Coast.

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

© Hekaya Initiative 2018-2020. All Rights Reserved. Design by Crablinks
%d bloggers like this: