
Malkia na Aishi Milele
Hassan Kassim
Imeandikwa na Hassan Kassim.
Nilitekwa zaidi na ufasaha wake, na jinsi alivyochambua mabadiliko ibuka katika ulimwengu wetu wa leo. Fikra ambazo sikuweza zifikia kimantiki hatimaye kwake zilimbainikia, akazifafanua na kuzianika kwa ulumbi usiomithilika. Tukahadithiana kuhusu nchi zetu, bara letu la Afrika, kwa ari ambayo hatimaye Waafrika huzungumza, kwa hisia na misisimko iliyoleta miamko ya uchungu, bila kutaradadi, lakini licha ya hayo, bado hatukusoma ndani ya hali yetu yasiyokuwemo. Tuliondoa tafarani ya kila namna na kuiangalia hali yetu kwa muono msafi.
Mithili ya mzazi aliyeona ndoto nyingi za kuotoa kumpitia mwanawe; mithili ya mwana, iliyomfikia upungufu wa babaze, uelevu wa maonevu waliyotendewa na wale waliojinasibisha na utetezi wa haki za kibinaadamu, jicho la kuigwa na kupigwa mfano wakitaka watupiwe wao. Jicho lao la bezo tulilolishuhudia kila uchao.
Tulizungumzia hali ya kusikitisha ya Libya baada ya kuanguka Ghaddafi. Tukahadithia Katanga, Sudan na Kenya, Uhabesha, Somalia na mwamko alioshuhudia katika nchi yake ya Eritrea. Tukatembea zaidi kwenye vichochoro vilivyofunikwa zaidi na kiza cha ukoloni, japo parwanja, ilijimudu kama siri; ni kama tuliambiwa tusiizungumzie vile na wale waliojikita kuwa wabora wetu wakifanya kila mbinu kufuta historia hii.
Mambo hupoteza mvuto wake yasipohadithiwa, na labda kwa kutohadithia ukoloni, wangeweza kusawazisha uwepo wake. Wakitujazia na maneno kama, ‘Lakini angalia maendeleo yote tuliyowaletea kama matunda yake.’
Tulizungumzia Waingereza, Wajerumani na Waitalia. Tukaelekeza nyoyo zetu Algeria, na unyama waliopitia kwenye mikono ya Wafaransa. Na kwa namna fulani, japo utajo wao huwa wa uhaba katika suala zima la ukoloni wa bara Afrika, tukazungumzia Marekani.
Hatimaye, tuliafikiana kama walivyoafikiana waliotutangulia kuwa Waamerika ndiyo waliokuwa na mikakati kabambe zaidi na waliozidi ugaidi katika wajihi wa dunia ya leo. Hakuna nchi iliyosalimika katika mikono yao hivi leo, ima kinyukilia au kisaikolojia. Hata hapo awali, baada ya vita vya dunia vya pili, walijipata katika njia panda, wakielekea zaidi katika kufuata mkondo wa himaya ambao ulikuwa kinyume na mfumo waliokuja nao waanzilishi baba wa nchi yao. Ukweli usiopingika hivi leo uliopigwa vita zaidi na wanaharakati Waamerika weusi kama vile Malcolm X na kilichokuwa chama cha Black Panthers. Na hata baada ya Raisi Nixon kuondoa mfumo wa kiwango cha dhahabu katika kukimu sarafu ya dunia, haikufichika kuwa uchumi wa dunia ulishikiliwa pekee kwa maguvu ya kijeshi ya Amerika. Hiyo ndiyo iliyokuwa nguvu ya kikweli ya dola. Na Japan walifahamishwa hilo. Kama vile China, Cuba na Katanga. Na waeritrea nao walishawahi kung’amua hayo tangu kadimu, Adal angesema. Kulikuwa na kite kati ya tabasamu zetu, na mmoja wetu, nadhani mimi, hatimaye angesema kuwa haya yote, wanavyoona wao huyafanya kwa udhuru wa demokrasia na maendeleo. “Nadhani huhalalishwa yote haya kwa udhuru kuwa mwishowe, nasi pia tutakuwa wanademokrasia.” Hapo ndipo Adal aliponigeukia na kuanza kusema jinsi alivyoanza sentensi zake zote, “Mwanangu…demokrasia si bidhaa.” Sentensi ambayo tungerudiarudia njia yote tukirudi nyumbani huku tukileta fikra zaidi ya hali halisia ya ulimwengu wetu wa leo. Demokrasia si kitu ambacho mtu anaweza kuzawadia na yeyote atakayesema maneno yanayofanana na hayo ni atuhumiwe na jambo lake liangaliwe vizuri zaidi. Kwani, Demokrasia haikuwahi kuwa bidhaa.
*
Malkia kafariki. Habari yanifikia katika nchi ii hii ambapo alipata habari kuwa amekuwa malkia. Watu kutoka kila pembe ya dunia wanasherehekea. Vichapisho motomoto vinatokea. Ewe Mungu nisamehe kwa kila tweet nitakayoicheka wikendi hii, anasema mmoja kupitia mtandao wa Twitter. Kwani huna hata heshima kwa maiti? Mwengine anamjibu. Kisha ujumbe mwengine unafufuliwa wa yuleyule aliyejibu hapo awali kuwa Afrika ilipopoteza mmoja wa wana wao, ilidiriki kuwa ilimtoweka hii heshima kwa maiti ambayo alionelea Malkia alistahiki, alidhihaki huzuni zao, na kudhihirisha wazi kuwa ilifaa hivyo kwani walikuwa wakimlilia muuaji na dikteta. Mechi zote za Ligi ya kiingereza zimeahirishwa. Kwa hiyo tuna wikendi ndefu kukaa na nafsi zetu na fikra zetu tata, tukazijumuisha zote na kuzilinganisha ni zipi zitakazoondoa ukoloni. Vurugu lihitajiwalo kuondoa lile vurugu lililozuliwa na ukoloni. Franz Fanon angeona fahari sana.
Ni mahusiano ya ajabu anayoshiriki mkoloni na aliyekoloniwa. Mahusiano yasiyobeba chuki kwa uhalisia wake bali hubeba shauku kuu ya kutojali. Ambayo nakisi huleta utambuzi tata kwa wakoloni wetu ambao waliona hizi misheni za ustaarabishaji, zigo asilo na budi ila kulibeba mzungu, kama inavyodhihirika katika shairi mashuhuri la Rudyard Kipling, ‘The White Man’s Burden, na hatimaye angeamka siku moja mbeleni kushuhudia dunia itakayomshukuru kwa utendakazi wake.
Mahusiano haya yanadhihiri zaidi katika nchi kama yetu ambako makovu ya ukoloni bado yanadhihiri katika baadhi ya wazee wetu. Kwani haujapita hata muongo mmoja tangu Mwingereza kukubali ukatili aliotenda katika muda wa ukoloni, ukumbusho wa hivi karibu zaidi ikiwa onyesho la channel 4, A Very British Way of Torture.
Nilikuwa na baadhi ya marafiki zangu wikendi hiyo, mmoja wetu akiwa Mmarekani, niliposema kwa utani kuwa, tulikuwa tunaomboleza siku hiyo, na hapo ndipo uafrika tuliouficha ndani ya nyoyo zetu haukunyapia tu bali ukaruka nje haswa. Waafrika wenzangu wakakemea vikali na kuniambia niteme mate kwa kufuru nilizotamka. Lakini kisha wakaangua kicheko, wakitambua kuwa ulikuwa mojawapo wa utani wangu, kusema mambo yazuayo hisia ili kupata nadharia zilizomo katika kikao hicho. Rafiki yangu Mmarekani alipigwa na mshangao kwa mazungumzo yaliyoendelea kuhusu kifo cha Malkia wa Uingereza, mazungumzo yaliyokosa hata chembechembe ya huruma na mandhari iliyokuwa ya kutojali, na ufichuzi wetu wa jinsi habari ilivyopokelewa dunia nzima. Wananchi wa Ireland wakiimba kwenye viwanja vya mpira, ‘Lizzy’s in a box, Lizzy’s in a box.’ ‘Elizabeth keshaingia sandukuni, Elizabeth keshaingia sandukuni.’
“Nasema, naelewa kuwa nchi yake ndiyo wakoloni wenu lakini hiyo haimaanishi kuwa ni sawa kusherehekea kuaga kwake?”
Na ni kweli. Hakuna kima chochote cha uchungu wa jadi kiwezacho kutoweka kwa miitikio kama hii lakini hatimaye ada ya ukoloni ni kutotukejeli na kutuelekeza jinsi itupasavyo kuhisi kuhusu matokeo kama haya. Tushaelekezwa vya kutosha. Rafiki yangu Mmarekani hakusema hilo kwa kejeli, lakini natamani ungeshuhudia nyuso za rafiki yangu waafrika kwa kutoelewa kwake uhalisia wa mambo. Wakaeleza zaidi kuhusu michango ya Malkia katika kuwezesha ukoloni, ukawa kama uwekezaji wa nchi yake. Kwani baada ya kikao cha Berlin cha mwaka wa elfu moja mia nane themanini na tano, Kenya ilikuwa mmojawapo wa miradi ya Ulaya kupitia British East Africa Company kama vile kabla yake nchi za Mashariki kama vile India zilivyoingiwa na kuporwa na British East India Company. Waliporwa kutoka India kuwa na uchumi mkubwa zaidi duniani zama hizo, takwimu zake kuwekwa katika trilioni nne, mpaka wakawaacha na madeni. Wakapora mpaka walipokosa cha kupora, wakapora neno la kihindi luut lililomaanisha kupora, likazua neno loot kwa kiingereza. India ikiwa kiungo muhimu sana kuelewa ukoloni kupitia mikono ya Ulaya, kama vile matukio ya Napoleon kuelekea mwaka wa elfu moja mia nane na moja katika Misri yakiwa muhimu sana kuelewa uanzilishi wa ukoloni katika dunia nzima. Huu ndiyo uliokuwa mtaji muhimu ambao tukizungumzia madola kawimu ya zama za jadi kama Abasiyya, dola la kimongol, dola la kimamluki na kisaljuki, madola yote yalienea mpaka kuishia Usipania, kilomita za kuhisabu kutoka mji wa Paris, lakini wasizidi kwani wakiona kuzidi kwao ni kuingilia maeneo yaliyo nyuma zaidi kifikra, maeneo yaliyo na hali duni sana, hali ya anga ikiwa baridi shadidi na theluji isiyoweza kustahamilika. Hata nusra shujaa Tariq ibn Ziyad aliamua kuifungua miji ya Usipania, kama Ketton na Toledo, na kwa ufunguzi huu, bara la Uropa likawa katika miaka yake ya mwisho wa giza. Kwa kutia taa ya kwanza ya barabarani Usipania, kukaleta mwanga kwa mara ya kwanza katika bara la Uropa na kufungua mengi zaidi kwao.
Kwani haukupita muda mrefu mpaka padri kwa kwanza kuwaruhusu kuingia katika miji hii iliyokuwa ya Kiislamu kwa miaka mia saba na kuwaruhusu kufaidika kwa elimu yao. Elimu ambayo nao walikuwa wameirithi kutoka Wagiriki kama Aristotle, Ptolemy na Plato. Elimu ambazo zilikuwa tayari zimeshafanyiwa tahakiki na wasomi majembe kama Ibn Haytham na Biruni, kazi za Aristotle zilizofanyiwa tarijama na Ibn Rushd waliyemwita kwa kiingereza Averoes, kwa miaka mitano kitabu Kanuni za Tiba cha Ibn Sina wakimwita Avicenna, ndicho kilichokuwa msema kweli katika Uropa nzima. Bali si Uropa tu, hata Christopher Columbus alipotoka Usipania, katika tokeo tunalolifahamu hii leo kama ugunduzi wa dunia mpya ambayo ikawa Amerika, alikuwa tayari ameshafaidika na vitabu vya kama Book of Roger maarufu cha Al-Masuudi wa zama zilizotangulia ambaye aliyekuwa ameshachora ramani ya dunia. Fununu za hii dunia mpya ikijulikana Mali katika Madola ya Songhai, miji kama Timbuktu waliokuwa wakwasi zaidi chini ya mfalme wao Mansa, ambao walishawacha athari katika hii dunia mpya. Wasomi wa zama zetu kama Jack D. Forbes na Ivan van Sertima wakiandika vitabu vya kitaaluma kuthibitisha hili. Hivyo basi wasomi wao waliobobea na waliojuwa wazi wa maneno haya walishuhudilia hilo, kama msemo maarufu wa Isaac Newton kuwa, “Hakika, tumesimama juu ya mabega ya majitu.” Na aghalabu hawahawa waliowafanyia hisani mwishowe wakawafanya kuwa watumwa.
Lakini tusikimbilie huko, mwanzo wa ngoma ni lele. Aghalabu madola haya yalianguka kwa kukataa kukubali mabadiliko ya dunia. Kwani Guttenberg alivyozuwa matbaa, walikuwa wa kwanza kuikataa, kwani ilitoka kwa watu dhalili kuwaliko. Na muda huohuo, Ulaya wakaikumbatia teknolojia hiyo ya uchapishaji. Elimu zikapatikana kwa urahisi mno, na ikaweza kuwasilishwa kwa kila mtu. Na kupitia elimu hiyo wakabadilisha hali zao. Kupitia elimu hizo wakajipata katika upeo wa dunia. Na pindi madola yale ya zamani yalipolazimishwa kufuata mkondo huohuo, walikuwa wamekwishachelewa. Elimu zikaendelezwa zaidi Uropa. Japo poda ya risasi ilitengezwa kwa mara ya kwanza katika dola la Kimughal, India, ni Uropa walioendeleza matumizi ya elimu hiyo.
Na elimu hiyo ndiyo Napoleon Bonaparte alipoingia nayo Misri, aliweza kuiteka kwa urahisi zaidi. Kipindi hicho, kati ya mwaka elfu moja mia saba tisini na saba, na elfu moja mia nane na moja, watu waligundua biashara iliyokuwa na faida zaidi, zaidi ya biashara ya utumwa iliyoendelea Marekani, na biashara ya ukoloni ikaanza. Miaka mitano ya mwisho wa karne ya kumi na tisa ikiona ongezeko kubwa sana la wageni katika jiji la Mombasa, wakitumia reli kupitia nyika iliyounganisha mji huo na ardhi zenye rutuba katika milima ya Kenya. Lakini kufika hapo walipatana na Wakikuyu, na wakang’amua fika ya kwamba kuwa hawangeweza kufanya lolote mpaka wawamalize Wakikuyu wote, na hapo ndipo vuta nikuvute ilipoanza. Maonevu yalipoendelea na ripoti zilizotolewa jiji la London kuwa tofauti kabisa na yale yaliyojiri humu nchini; na kwa kufichwa kwa hali ya juu, hayangetambuliwa mpaka tukio la ‘Hanslope’s disclosure’ katika miaka ya elfu mbili na kumi ndipo yalipojulikana kuwa viongozi wote Ulaya walifahamu matokeo yote yaliyojiri huku nyumani.
Na maovu waliyopitia babu zetu, japo Malkia alifahamu uwepo wake, aliyafumbia macho na kutofanya lolote kuondoa udhalili uliowavaa. Nasi basi hatukuwa maridhia kama mababu zetu, walioinamisha vichwa vyao Mzee Jomo Kenyatta aliposema, “Sote tumepigania uhuru, sasa tujenge nchi.” Hatuwezi wacha yaliyopita yakawa ndwele ilhali kila kukicha yanatudiriki athari zake katika mifumo ya hivi leo. Ikiwemo katika mipango yao ili tuwaelekee kama wafadhili wetu ili tusifahamu ukandamizaji wanaotufanyia kama ukandamizaji.
“Mwamzungumzia kama ni Hitler!” Rafiki yangu Mmarekani akasema.
“Tukiangalia kwa kweli,” nikasema polepole, “kwani tofauti iko wapi?”
Akaniangalia kwa upeo wa kushtuka, kama nilimtishia vile. Kwa muda huo, nadhani alinifikiria mtenda dhambi ya kupinga maonevu ya wamayahudi.
“Sisi pia tuliwekwa katika kambi za mateso,” nikaongeza, naye akaangalia kando tu.
“Kunradhi, poleni,” akasema, chini ya pumzi zake, “Sikujuwa hilo.”
Wala hakuna ajuae. Hekaya za magofu ya mwisho ya himaya ya Ulaya hubakia maelezo ficho, ya chini kabisa katika historia. Elimu yetu ya kikoloni huzimua athari za ukoloni, na ni tu kwa kukuwa kwa kifikra na kuvumbua kazi muhimu kuhusu mada hii kama mshindi wa Pulitzer Caroline Elkins’ Imperial Reckoning ambapo taswira kamili huanza kuzama akilini. Kazi hii imebaki nami tangu niisome na ikanipa msukumo zaidi katika mabaraza ya kujinasua na ukoloni. Nimejitumbukiza ndani sana mpaka sasa katika mitandao yangu ya kijamii, Twitter tuseme, imejaa vichapisho vya waafrika, Wahindi, Wamashariki waliochoshwa na taasubi za kimagharibi katika hali zake zote ibuka, ukoloni mamboleo na upekee wa kimarekani, mitazamo isiyokuwa ya kiafrika, na kuwashuhudia hawa watu wakiitisha na kuchukuwa nafasi zao ambazo walinyimwa hapo awali. Mazungumzo ambayo usukani wake si hisia pekee lakini ya kitaaluma na inafurahisha sana kuona.
Kupitia mwonekano wa mkoloni, kama Lord Cromer vile tuseme, ama uchambuzi wa ukoloni kama ulivyofanya na Franz Fanon, tunajipata ana kwa ana na ukweli fika ya kuwa haikuwa nia ya mkoloni kukaa nasi milele. Tuchukulie mfano wa Misri. Madhumuni tangu mwanzo yalikuwa kutusukumizia kwa ubabe na ubepari wa ubora wao, watuvue lugha zetu za kiafrika, mila, maadili yetu, na yote tunayoyaenzi na kwa mbadala watutwike yao. Hiyo ndiyo maana shule zikawa viungo muhimu vya kutwika mfumo huu. Na kama tutadadisi kihaki, tutapata kuwa mkoloni alishinda katika maazimio yake, na ushindi wake ndiyo ulioleta utandawazi. Mwisho wa kwisha, tuliambiwa ukoloni ulikwisha kwa kuondoka kwa Mwingereza, lakini mbadala wake tuliachiwa magofu ya waafrika waliobeba mienendo yote ya kiingereza ndiyo watuongoze. Mwafrika aliyefanywa mwingereza. Asiyethamini uafrika. Ngozi nyeusi lakini kinyago cheupe. Hata kama tungesema kuwa walijaribu kukimbia hiki kivuli cha ukoloni, hawakuweza kwani kuna athari kubwa moyoni kwa kufutana mabega na watu. Kama raisi wetu wa kwanza Jomo Kenyatta, uonekanao wake wa wazi kabisa katika filamu aliyoiga katika miaka hiyo akiwa ughaibuni, Sanders of the River, kama chifu wa kijiji kimoja cha kiafrika na gavana mmoja wa kiingereza ndiye aliyekuwa mizani iliyomwonyesha usawa. Na inasemekana uongozi wake ulikuwa vivyo hivyo, akielekea ulaya kama ramani kamili ya uongozi. Mwishowe walifikia maazimio yao ya kikoloni. Wakamvua Mwafrika mpaka dini yake pia. Uwezeshwaji wa Wanawake wa Kimisri, Kiraini, Kialgeria, ukawafanya watupe mbali hijabu zao, athari ya wazi zaidi ya jamii yao. Kuna msemo katika insha moja ya Franz Fanon, Algeria Unveiled, ibara yenye athari ya, ‘Huyu mwanamke aonaye bila ya kuonekana humuogofya sana mkoloni.’ Tukakabiliana kwa kiwiliwili na utaifa; ukashurutishwa, umashariki athari yake ikafututiliwa mbali kabisa, ustaarabishaji ukakamilika, ukashajiishwa na ukawa ndiyo mkondo. Ndiyo uhalisia lakini?
Jambo la kustaajabisha lilitokea katika miaka ya themanini. Kizazi kipya, hata kisiwe na msukumo wa kushikamana na dini, wengine wao wakiwa na ujabari tu kukiuka waliokandamizwa nayo baba zao, tarakimu za kustaajabisha za wanawake walivaa hijabu kwa mara nyengine na kugutusha wakoloni kote waliko. Wangechaguaje kurudi katika vazi la kudhalilisha ambalo azima yao ilikuwa kumnasua mwanamke kupitia ukoloni? Vazi lililomkandamiza mwanamke na kumnyima uhuru wake? Wangetupaje huria na uliberali kwa mikondo hiyo iliyopitwa na wakati? Vipi?
Na hivi leo nikishuhudia kizazi changu katika juhudi zake chungu nzima, wakifufua na kuhifadhi lugha zao, wakikufuru miungu ya kilimwengu, siasa za utambulisho zikipigwa msasa, fikra inanijia… Kukata shina la mti huenda ukashajiishwa kama utendakazi mzuri, ikaleta taswira ya ushindi wa vita vya kisaikolojia, lakini aghalabu, mizizi hukita na kuzama chini zaidi, shina likanawiri kwa mara nyengine, matawi yakazaa vitagaa, yakazaa halaiki ya majani, yakanong’onezana. Na mwia si mrefu kabla ya hisia za mvutano zikaibuka na hatimaye zisimbakishe mtu. Minghairi ya taswira ya jamii zetu kuvuka unyama waliotendewa, kuna kifani ya vijana wawili wa Kialgeria, mmoja miaka kumi na tano na mdogo wake kumi na tatu, waliomuua kijana mwenzao wa kifaransa umri huohuo, rafiki yao ambaye walikuwa na mazowea ya kucheza naye. Walipoulizwa ni kwa nini walifanya hivyo walijibu kuwa ni lile waliloweza kufanya kwa uwezo wao kama jawabu lao kwa ukandamizaji mababa wa yule Mfaransa aliowafanyia mababa zao. Ndiyo maana wakamdunga kisu. Kesi hii katika The Wretched of the Earth inafaa kuwa ibra kubwa kwetu hivi leo kuhusu hisia azibebazo kila asiyekuwa mkoloni kwa wakoloni wake, ima awe mtoto ama kinyanya aliye mbali na nchi yake. Na katika haya mazungumzo na marafiki, au watu ajinabi tukibarizi na vikombe vya kahawa, au katika matumizi bora zaidi ya mitandao ya kijamii, hatua tunazichukua kuelekea kule tunakostahiki kuelekea. Japo utambulisho ni swala tata katika ulimwengu wa utandawazi, ilimradi tunajitambulisha kama tunavyotaka wenyewe, ilimradi kalamu tumezishika wenyewe, tunaelekea pahali.
Aristotlr, Averoes, Columbus, Guttenberg, kiswahili, Mozilla Foundation, Napoleon, Plato, Ptolemy