Wanyika Nyikani

“Mama…?” alimaka Wanyika baada ya kuitwa na nyanyake na kuelezewa kuwa mgeni aliyewasili alikuwa mamake mzazi.

Jua lilikuwa limewaka sana na ulikuwa ni msimu wake wa  mwezi  wa Januari ambapo jua huwaka bila msamaha. Lilichoma   kila jani, mimea ikakauka, shamba likabaki kavu na udongo kupasuka pasuka na kufanya machimbo makubwa makubwa kama mikorongo nyikani.

Mchana huo, Wanyika alikuwa akisanya mizizi ya viazi vitamu angalau yeye na nyanyake wapate chajio. Imekuwa ni siku ya nne sasa kabla ya kupata chakula cha haja cha kujaza matumbo yao. Mara nyingi walikunywa maji ya moto tu ili kudanganya matumbo yao na kulala. Na asubuhi ilipofika mpango ulikuwa ni kusaka vibarua kutoka kwa majirani angalau wapate posho. Haya ndiyo yaliyokuwa maisha ya  Mgange Nyika, wakati wa msimu wa kiangazi. Matajiri walitoa  vibarua aina kwa majirani zao na kuwapa kibaba cha posho kama malipo badala ya ngwenje.

“Huyu ni mamako mzazi,” Nyanya alimsisitizia Wanyika. Maajabu ya Musa, ukistaajabu ya Firauni utayaona ya Musa. Wanyika msichana mkubwa sasa wa miaka saba, hajajua maisha mengine ila yale ya uchochole akiwa na nyanyake pekee. Maisha ya sina sinani, ukiulizwa husemi. Umaskini wao ulikuwa wa aina yake, hadi mafukara wa kijijini waliona aibu kujisuhubisha nao. Kila walichokuwa nacho  kiliashiria umaskini, si nyumba yao ya udongo,  wala paa waliloezeka kwa mabati makuukuu bali kila kitu kiliashiria ulalahoi wao.

“Wanyika,” mamake aliita baada ya kimya kutawala. Kweli kimya kingi kina mshindo na naam, Wanyika alimkodolea macho mamake tu kwa muda wote huo. “Mwanangu…” alisema mamake Wanyika huku akimkumbatia na kutokwa na machozi. Alimfumbata Wanyika kwa muda, wakakamatana wote wawili. Lakini Wanyika bado alikuwa na hisia mseto, alimkodolea nyanyake macho, alikuwa amesimama mkabala naye kana kwamba anataka kufunguka hivi, lakini wapi!

“Mimi ni mamako mzazi,” alipumua, huku akimdadisi Wanyika kama simba mla watu anayekagua windo lake kabla ya kulirarua vipande vipande.

Ilikuwa mnamo mwaka elfu-moja, kenda-mia na sabini ambapo Maria akiwa darasa la sita katika shule ya Mtakatifu Hannah alikutana na kijana mtanashati aliyejulikana kama Pius wakati wa michezo ya riadha. Ulikuwa ni muhula wa pili kipindi ambacho mashindano ya riadha na michezo mingine yaliendelea. Pius hakupenda sana riadha na wala hakujishughulisha na mchezo wa aina yeyote ule.Yeye alipenda sana masomo. Alikuwa wembe masomoni akihifadhi nambari moja bila upinzani wowote. Alikuwa mwanafunzi katika Shule ya Upili jirani ya Mtakatifu John.

Pius katika pitapita zake ndipo alikutana na Maria aliyekuwa amejikalia ovyo kwenye kivuli kilichotolelwa na mti wa mwembe.

“Hujambo dada!”

“Sijambo.”

“Mbona umejitenga na wenzako…unaumwa?”

“Ah… sina neon,” alijibu, huku akijitia hamnazo.

Pius alimkaribia pale alipokuwa kivulini.

“Nimesema sina neno mbona hunisikii!” alikasirika Maria.

‘Aaa…usiwe hivyo dada mimi sina ubaya wowote nawe ni salamu tu. Sikunuia kukuudhi samahani basi. Mimi pia naona nimebinyika kiasi. Naona pia wewe huipendi michezo hii. Haikupi shangwe,” aliyasema maneno haya kama tayari ameketi karibu naye pale kivulini.

Maria aliogopa kuonekana na kijana akiwa mbali na wengine.Ilikuwa mwiko kwa msichana kuonekana na mvulana peke yako.Angechukuliwa kama kibiriti ngoma. Maria ni mhafidhina.

Mara Maria akaamka ghafla na kutaka kuondoka pahali pale.Pius kamdaka mkono na kumvuta karibu naye .Maria hakukaidi kwa sababu ya kuogopa kuzidisha mvutano kati yao .Akatii amri na kuketi.

Pius alipata nafasi tena ya kujijulisha kwa Maria kwa mara ya pili. Maria naye hakuwa na budi ila kujitambulisha pia na kumueleza mwenziwe sababu yake kukaa peke yake pale  kivulini. Alikuwa anajihisi mgonjwa – kichwa kilikuwa kinamuanga sana. Ulikuwa ni wakati wake ule wa mwezi lakini hakutaka kumfunulia  Pius hayo yote.Alimwambia kuwa ni kichwa tu ambacho kilikuwa kinamuanga.

Pius kusikia hivyo alitoka hapo akaenda madukani kumnunulia dawa ya kuumwa na kichwa. Hivyo ndivyo urafiki wao uliaanza. Lakini urafiki ukavuka mpaka na wakawa wapenzi. Mapenzi yakakita mizizi katika kipindi cha likizo cha mwezi wa Agosti. Muhula wa tatu ulipoanza bado wawili hawa  waliendelea na mapenzi yao  kwa njia ya barua .Wakati wa likizo la Disemba walikutana ,wakalishana kiapo kuwa penzi lao litadumu milele.Ni msimu huu ambapo alipatikana Wanyika.

Maria alikatiza masomo ili kulea mimba ya Wanyika. Upande mwengine naye Pius alipogundua kuwa penzi lao la siri limetibuka na matunda yake kuonekana na walimwengu, alimkana mwenziwe na kusingizia kuwa yeye gumba na hakuwa na uwezo wa kumpa haragwe banati yeyote yule. Ilimbidi Maria kujikaza kisabuni na kulea mimba ya Wanyika bila usaidizi wa Pius.

Maria alipojifungua mtoto Wanyika aliamua kumuacha chini ya ulezi wa mamake mzazi na kufunga safari yakuenda Mombasa ili kutafuta kazi ya uyaya anagalau apate uwezo wa kumuangalia mamake mzazi na mwanawe. Alifanikiwa na kupata kumfanyia mhindi moja kazi ya nyumbani, japo kazi yenyewe ilikuwa ni ya sulubu, alijikaza kisabuni na kuwajibika. Wakati mmoja alipokuwa anaenda sokoni Kongowea kununua mboga na vitu vyengine kwa ajili yakutayarisha mapishi alikutana na kitana mmoja na wakatokea kuwa marafiki. Usuhuba wao uliendelea kwa muda, ikawa wanakutana mara kwa mara. Kila walipokutana ukuruba wao ulizidi, hatimaye kitana yule aliamua kufunguka na kumueleza Maria yale yaliyokuwa moyoni mwake, kwamba anampenda sana na angetaka sana wawe na uhusiano wa kimapenzi. Maria naye hakusita bali alimueleza kinaga ubaga ukweli wa mambo, kwamba yeye sio mwari na ana mtoto mdogo wa miaka saba anayeishi na mamake mzazi, na wawili hao walikuwa wanamtegemea yeye . Kitana kwa upande wake hakuona tatizo lolote, ila alkikuwa na sharti moja tu! Wanyika angebaki na nyanyake. Kitana hakuwa tayari kuchukua jukumu la kumlea mtoto wa Maria ambaye si damu yake. Maria alikata kauli na akaamua kuipa nafsi nafasi nyingine ya kuwa katika mahusiano. Mda si mrefu walifunga ndoa na Maria akaacha kazi yake ya nyumbani aliyofanya kwa jumla ya miaka saba. Maria na mumewe makaazi yao yakawa Jomvu, wakiishi kama mume na mke rasmi.

Miezi miwili ndani ya kuishi na Kitana, Maria aliamua kwenda nyumbani kwao na kumjuza mamake kuhusu mahusiano yake mapya na pia kumjulia hali mwanawe baada ya miaka saba ya kuishi Mombasa.

Wanyika hakufurahishwa na ujio huo. Aliishi miaka saba! Aliishi miaka yote hiyo bila ya fununu yoyote kuwa  alikuwa na ‘mama,” tofauti na nyanyake, ikawaje tena leo pakaja mwanamke mwingine nakujidai eti ni mamake mzazi? BI Chao hakuwa mlezi wake tu bali alimfahamu kama mamake mzazi  na hata kumpa jina la kupanga –“atele” –Jina hilo  halikuwa na maana yoyote maalum ila ndivyo walivyoitana mtu na bibiye.

Baada ya kusimuliwa kisa chote, Wanyika alipukuruka mbio nje hadi nyuma ya nyumba yao akilia akiwa na mchanganyiko wa hisia. Si furaha si huzuni. Alikuwa katika hali ya taharuki. Alikimbilia mafichoni mwake alikoenda kujifariji, kujiliwaza, kuomba au kusoma alipopata wakati. Alikaa huko kwa muda na akakata kauli kuwa hangejihusisha na “mama’ huyo kivyovyote na kumwacha bibi yake.

Maria hakukaa sana kijijini baada ya kuona kuwa hapakuwa na uwezo wowote wa  kumshawishi  mwanawe kumtambua kama mamake mzazi. Alirudi Jomvu, Mombasa kwa mumewe . Mamamke hakupinga uhusiano wake na Kitana ila alishauri wawili hao uhusiano wao utambulike kirasmi na watimize mambo ya kimila.

Zikapita siku nyingi sana tangia kuondoka kwa mamake mzazi Wanyika. Maisha ya Wanyika na nyanyake yaliendelea kuwa ya kutamausha lakini Wanyika hakukata tamaa kamwe. Walifanya vibarua kukidhi mahitajii, wakavuna mavuno wakati wa masika na mjombake ambaye alimfadhili masomoni pia. Licha ya changamoto zote, Wanyika alikuwa wembe shuleni akawa kivuli cha babake, Pius ambaye alikuwa hajawahi kumwona ila kumsikia tu. Wanyika alisoma hadi kidato cha sita yani (KACE) wakati huo. Alikuwa katika shule ya bwenini na aliutumia wakati wake kudurusu kwa bidii.

Siku za kutembelewa wanafunzi na wazazi wao zilimpata Wanyika maktabani akijisomea kwani hakuna aliyekuja kumtembelea. Ila siku moja kati ya siku za kutembeleana mwandani wake Peninah alimwita, “Wanyika , Wanyika?”

“Eee,” alijibu.

“Una mgeni nimetumwa nikuite na mwalimu wa zamu,” alisema Peninah.

Akashtuka. “Mimi nipate mgeni…mgeni atoke wapi! akajisemea kimoyomoyo. Anakosomea kulikuwa mbali na nyayake anakoishi na hangeweza kuja kumuona. Akawa ana maswali na kibao moyoni kuhusu mtu huyo aliyekuja kumtembelea

“Ni nani huyo…,” aliwaza  hayo alipokuwa akitembelea nyuma ya Peninah haraka haraka.

“Wageni wako wapo kwenye ukumbi wa shule,” Peninah aliendelea kusema. Alimfuata kimya. Ndani ya ukumbi alimwona mjombake akiwa na mtu  mwingine mfupi, mweusi, mnene na aliyekuwa amevaa kweli kweli! Hamna shaka mtu huyo alikuwa tajiri kulingana na mavazi yake, hata alining’iniza funguo za gari katika vidolee vyake. Wanyika alijaribu kuvuta kumbukumbu, kwa matarajio kwamba aweza kumjua jamaa yule. Lakini wapi hakupata!

Mjombake hajawahi kutembelea shuleni abadan japokuwa yeye ndiye aliyekuwa na jukumu la kumlipia karo Wanyika. Baada ya salamu, Wanyika alijulishwa kuwa ujio ule ulikuwa ni wake na yule jamaa aliyeandamana na mjombake alijulikana kama Pius na ndiye babake mzazi. Alimaka, akashangaa na akashtuka!

“Eti !Baba? Babangu?” Haijawahi mtokea siku moja kwamba angekutana na babake mzazi hata ndotoni hajawahi kumuota. Nyanyake alikwepa swala la babake mzazi kila alipomuuliza; leo iweje katokea jamaa na kudai kuwa ni babake mzazi? Hisia kinzani zilimvaa, hakujua afurahie au alie kwanza. Alibaki kuchanganyikiwa…

Babake alipomuona yupo hoi alimdaka mara moja na kumpaa kiti akae kabla hajaanguka kutoka na hisia mseto zilizomvaa. Pius akamueleza matokeo yote, tangia kupatana na mamake Wanyika, msiba uliowapata na kupelekea kuvunjika kwa penzi lao. Lakini Pius hakuwa mkweli akaongezea na ya kwake. Alidai alimposa mamake Wanyika lakini akakataa ombi lake na ikaampelekea yeye kumuoa mwanamke mwengine na sasa ana familia naye. Kwa jumla alizaa naye watoto tisa! Hilo lilimshangaza Maria lakini halikuwa linamhusu kwa sasa.

Maria aliwaangalia wote wawili kwa macho makavu, maelezo yale yalimchoma lakini hakuwa na budi yaliyopita ni ndwele. Lililomchoma zaidi ni jinsi alivyokula mwande ilhali ana baba aliyekuwa na uwezo wa kumpa maisha mazuri. Alizama katika mawazo, wawili wale waliongea lakini alikuwa hayupo pale, katekwa kitambo na mawimbi ya mawazo chungu mzima. Baada ya muda mjombake alimuashiria amuandame hadi katika gari la babake, aina ya Toyota. Akafungua buti ya gari na kumtolea Maria mapochopocho na zawadi zengineo. Maria alivipokea japo shingo upande na kufufliza hadi bwenini na kukosa hata kumshukuru babake mzazi.

Kumbe wakati huo wote Peninah alikuwa amekalia gogo mkabala na ukumbi wa shule akitazama sarakasi yote. Alikimbia bwenini na kumpokea zawadi Wanyika. Kumbe alikuwa na lake, akaanza kumuuliza maswali Wanyika. Wanyika akashindwa kujibu, maana yalikuwa yanaandamana moja baada ya jingine bila mapumziko.

“Peninnah! Peninnah! Naomba unipe muda nitulie,” alimwomba Wanyika, Peninah naye akamuelewa. Bila ya kusita Wanyika alijibwaga kitandani na kupumzika. Baada ya muda aliinuka na kumueleza mwandani wake yale yote yaliyotokea. Peninah alishangazwa na tendo la Pius la kumtelekeza mwanae kwa miaka yoye hiyo. Swali hilo la Peninah lilizidi kumchoma Wanyika lakini hakuwa na la kufanya bali kumeza machungu tu!

Siku na masiku yakasonga, Wanyika akakalia mtihani wake wa Kitaifa wa kumaliza shule. Alipoumaliza akarudi nyumbani kwa bibi yake na kumueleza matukio yote yaliyompata. Bibi alizipokea habari hizo bila mshangao wowote! Wanyika akajiuliza, “Je alikuwa anayajua yote haya?” lakini wapi, hakupata jawabu.

Wakaendelea na maisha yao ya uchochole, vibarua hapa na pale. Wanyika akajitahidi zaidi na kupata kibarua kama mwalimu wa shule ya msingi, japo ilikuwa ni kazi ya muda ya kushikilia aliyopata bila cheti. Majibu ya mtihani yalitoka na alifaulu vyema, azma yake sasa ilikuwa ni kujiunga na chuo kikuu. Pale shuleni alishikilia kwa mihula miwili na akapata barua kutoka kwa babake mzazi. Alimtaka amtembele mjini Mombasa ili apate kujua nduguze wengine. Akamfahamisha nyanya na mjomba kuhusu mwalikule. Wakamuhimiza aukubali naitakuwa vyema kwake yeye Wanyika kujua familia yake nyengine. Alikata shauri na kukubali mualiko ule wa kwenda Mombasa.

Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufika Mombasa na babake alimsubiri katika stendi ya Mwembe Tayari. Akampeleka nyumbani na kumkaribisha vyema, ila mamake wa kambo hakupenda ujio wa Wanyika, na hakuficha hisia zake katu. Wanyika akaliona balaa likijileta, mamake wa kambo hakutaka ale na wanawe hata pia kuongea. Wanyika akaona asijiumize roho, akasubri siku babake yupo nyumbani na kumueleza kila kitu. Akamuomba amtembeze Mombasa, maana alikuwa na hamu nayo. Babake akampeleka kuina bahari ya Hindi, ilikuwa mara yake ya kwanza na alifurahishwa sana na jinsi mawimbi yalivyojibeba yakitupana bwelabwela!

Jioni moja baada ya chajio, Wanyika alimuita babake kando na kumuelezea dhamira yake ya kutaka kurudi bara. Maisha ya mama wa kambo yalikuwa yamemshinda na kachoka kuvumilia. Babake kwa roho safi alimkubalia ombi lake. Asubuhi yake alimuandalia zawadi za kupeleka bara na kumpeleka stendi. Wanyika akaabiri basi na kuanza safari yake ya kwenda bara. Lakini kuna jambo lilombughudhi. Katika ujio wake wa pwani alipata kuwahi kufanya urafikina kijana mmoja muuza madafu aliyefahamika kama Odour. Siku chache zile alizokuwa Mombasa, alitokea kumpenda kijana yule. lakini kafanya kosa la kutomuaga kijana yule na kumuelezea hisia zake.

Nyumbani akapokelewa vizuri na nyanyake, na alikuwa na hamu ya kuelezwa kuhusu habari za Mombasa. Waliongea wawili hao hadi usiku wa manane. Walikuwa wamepezana sana. Mapenzi baina ya bibi na mjukuu wake yalidhihirka. Hatimaye machovu yalimfika Wanyika na usingizi ukamtwaa kwa pupa akishtuka ni machweo akiamshwa na bibiye.

Asubuhi ile Peninah, mwanafunzi mwenziwe na jirani yake kule bara alirauka kwa kina Wanyika ili kumuuliza kuhusuu habari za Mombasa, naye Wanyika hakumficha alimuueleza yote mpaka kuhusu muhibu wake Oduori. Peninah alifurahhshwa na habari zile, nako huko Mombasa Oduori alimuulizia Wanyika kutoka kwa ndunguze, akaambiwa Wanyika si wa Mombasa tena na alirudi zake bara kitambo. Oduori alihuzunsihwa na habari zile, lakini akaomba anwani ya Wanyika na akapewa.

Wanyika kule bara alitamani sana azisahau kumbukumbu za Oduori, maana alijua kuwa hatosamehewa na muhibu wake. Lakini barua ya Oduori ilimfikia, kwa mshangao alichana bahasha na kuanza kusoma barua ile…

SLP 2067

MOMBASA.

Kwa muhibu wangu,

Wingi wa salamu.Natarajia barua hii itakupata ukiwa buheri wa afya.Mimi pia ni mzima ila wasiwasi kwako.

Muhibu wangu, nilipata habari kuwa uliondoka bila hata kuniaga. Nilijibiidisha nikaipata anwani yako kutoka kwa dadako Sarah. Mbona ukafanya hivyo?

 Wanyika, lengo la kukuandikia barua hii nilitaka nikukueleze kuwa, mara nilipokuona moyo wangu ulitokea kukupenda na nilitaka uwe wangu wa maisha. Na tafadhali usinikatalie ombi langu.

Mimi wako mpenzi,

Oduori.

Barua hiyo ilidhibitisha hisia za Wanyika kwa Oduori, maana aliipokea kwa furaha. Oduori akawa mpenzi wa kwanza wa Wanyika. Akafanikiwa kujiunga na chuo kikuu baada ya muda mfupi. Alienda kusomea ualimu, na chuoni Oduori mara kwa mara akawa namtembelea Wanyika. Wanyika akaona bora mapenzi yao yasiwe ya siri tena, na akapanga mkutano pande mbili zikutane ili watambulishwe rasmi. Japo ya tofauti za kikabila na kimila baina Wanyika na Oduori, wazazi walibidi waghairi japo shingo upande na kukubali mkutano huo. Baada ya chuo kikuu, kibali na baraka kutoka kwa wazazi wawili hao waliowana na kuishi raha mustarehe. Kwa kweli wa nyika halii nyikani akashiba, hata pwani atawinda tu!

 

 

.

 

 

.

 


Leah Odungo

Leah Wanyika mzaliwa wa pwani na mwandishi chipukizi wa hadithi za hekaya. Alisomea ualimu katika chuo kikuu cha Moi.

Comment

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

© Hekaya Initiative 2018-2020. All Rights Reserved. Design by Crablinks
%d bloggers like this: